Kiumbe dhaifu: Siyo haki kuyasahau mauaji ya kina Sharon Otieno na wenzake

Mamake marehemu Sharon Otieno akifarijiwa (kati) na jamaa zake baada ya kupokea habari mwanawe ameuliwa.

Mwanamke, Mwanamke ni kiumbe wa ajabu aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu bila ya makosa na tashwishi zozote. Mwanamke, zaidi sana anaashiria pambo katika ulimwengu.

Ni kiumbe kinachostahiki kuonyeshwa upendo, kuhudumiwa bila ya vuta ni kuvute, kwa kuwa ametokana na ubavu wa manamume. Aghalabu, ni kinaya kuwa kutokana na huyo huyo mwanamume, kunakuwa ni chanzo cha kunyanyaswa kwa wanawake.

Iweje Mwenyezi Mungu atuumbe kutokana na ubavu wa mwanamume kisha mwanamume huyo awe ndie chanzo cha maudhi na mateso katika maisha ya mwanamke? Kwa muda mrefu sasa wanawake wamekuwa wakipitia dhulma za kila aina katika maisha yao ya ndoa, badala ya ndoa kuwa chanzo cha furaha kwao kinakuwa chanzo cha huzuni kubwa katika maisha yao.

Tulidhaniya kuwa tamaduni za kiafrika pekee ndizo zilizokuwa zikichangia katika kuwakandamiza wanawake, lakini pamoja na maendeleo tuliyofikia bado wanawake wa kiafrika wameendelea kuwa kama watumwa, kumtumikia mwanamume na watoto paka hatima yao. Miaka ikasonga na wanawake wakapata vyeo katika nyadhfa mbali mbali, wanawake wakaelimishwa na mpaka sasa wanawake wengi wamo katika vyeo vikuu vya serikali.

Gavana wa Migori Okoth Obado alipofikishwa mahakamani kwa madai ya mauaji ya sharon. Aliwachiliwa kwa dhamana.

Kupata elimu hakuja mnusuru mwanamke kuendelea kupitia unyama. Hivi punde kesi za kinyama zimegonga vichwa vya habari. Wanawake wanapatikana wakiwa wameuawa katika hali za kutatanisha na za kuhuzunisha.

Mwaka jana Sharon Otieno, msichana mwenye umri wa miaka 26 alipatikana ameuawa katika hali ya kusikitisha zaidi kwa kuwa alikuwa na uja uzito wa miezi saba. Kijusi chake pia kilinyimwa uhai na makatili hao.

marehemu Sharon Otieno aliyeuawa kinyama na mwili wake kutupwa kichakani.

Mauaji ya Sharon yalienea kila mahali kutokana na mahusiano yake na gavana wa Migori Okoth Obado. Bw. Obado akazuiliwa siku 33 na kuachiliwa kwa dhamana. Kesi yake itaendelea kusikilizwa mwaka huu, mei tarehe sita hadi kumi na saba.

Huo haukuwa mwisho wa vifo vya wanawake, ikawa ndio mwanzo wa kuuawa kwa wanawake nchini. Ukawa ni ukurasa mpya uliofunguliwa wa mauaji ya wanawake. Bi Monica Nyawira Kimani akafuatia. Bi Nyawira alikuwa mwana biashara wa miaka 29. Mwanamke mwenye bidii sana, ila akakutana na hatima hiyo mbaya sana.

Marehemu Monica Nyawira aliyepatikana ameuawa chumbani kwake eneo la Milimani

Alikutwa ameuawa katika bafu la kuogea na kaka yake ambaye alikuwa na wasiwasi baada ya kutomuona dadake kwa siku kadhaa. Bi Nyawira alikuwa amepanga kwenda safari lakini hakuwa na mawasiliano na kaka yake wala wazazi wake.

Ilimbidi kaka yake kwenda nyumbani kwake akaone ni kipi kilichomsibu dada yake. Washukiwa wakuu wa kifo chake Bi Jacquline Maribe na  Bw Joe Irungu walifikishwa mahakamani. Swali ni je Bi Monica atapata haki kwa maovu aliyotendewa? Unapoamua kumtoa uhai binadamu mwenzako, akilini mwako unaona kuwa unemtendea haki?

Joe Irungu mshukiwa mkuu wa mauaji ya Monica Nyawira.

Tusikomee hapo, mwaka wa 2019 umekuwa mwaka wa vifo vya wanawake kutoka mwanamke mmoja hadi mwengine. Vifo visivyojulikana kiini chake ni nini. Kuwa katika jinsia ya kike kumekuwa kama laana isiyo na dawa.

Bi Mildred Odira, mfanyikazi wa ‘Nation Centre’ mwanamke ambaye alikuwa ameripotiwa kupotea kuanzia Januari tarehe29 alipochukuliwa na dereva wa texi ili apelekwa hospitali akapatikana katika chumba cha kuhifadhia maiti cha ‘city’.

Mwili wake ulikuwa na majeraha ya kuonyesha kana kwamba Mildred alikuwa amegongwa na gari. Dereva wa texi hiyo ndiye mshukiwa mkubwa pamoja na askari gongo aliyeita texi hiyo. Inasikitisha kuona mwanamke aliyemwacha mwanawe wa miaka tisa katika kifo cha hali kama hii.

Marehemu Mildred Odira aliyepatikana kauliwa barabarani.

Swali ni, nani aliyeupeleka mwili huo katika hifadhi hiyo ya maiti? Ni bora kila mwili unaopelekwa katika hifadhi hiyo kukaguliwa na kujua ni nani aliyeupeleka mwili ili kuepuka kesi kama hizi. Kifo cha Bi Mary Kamangara ni cha kutamausha sana.  Uishi na mume wako kwa siku nyingi na dhiki nyingi za kuvumilia mitihani ya ndoa, mwisho unauawa na mpenzi wa mume wako.

Dereva wa texi Michael Githae Mathenge aliwapeleka polisi mahali walipoutupa mwili wa marehemu Mary.  Uchunguzi wa kifo chake ulidhihirisha kuwa Mary aligongwa kichwani mara tisa, na chombo kilichokuwa na makali, na kuchangia kupoteza kwake fahamu.

 Mume wake bwana Joseph Kori aliachiliwa baada ya kuzuiliwa ili upelelezi uendelezwe na maafisa wa uchunguzi, ilipojulikana kuwa hakuhusika katika mauaji hayo, ila ni mpenzi wake Bi Judy Wangui aliyetekeleza mauaji hayo.

Hivi juzi msichana wa kidato cha tatu alipatikana ameuawa katika lodge, katika  Kaunti ya Narok. Msichana huyo alikuwa mja mzito. Kichwa cha msichana huyo kilipatikana kikiliwa na mbwa.

Mary Wambui aliyeuliwa na mwili wake kutupwa

Inasikitisha sana kuona nchi yetu ya Kenya inakumbana na matatizo makuwa kama haya. Wananchi wamekuwa magaidi kupita kiasi. Ugaidi sio tu kubeba mabomu na kulipua watu katika barabara na mikahawa, la hasha, pia huu unatambulikana kama ugaidi. Ni tendo la kigaidi kumtoa mtu uhai, ni tendo la kigaidi kumuua mtu kwa njia ya kinyama kama hii.

Mwanamke mwengine naye apigwa kipigo cha nyoka na mume wake eneo la Kahawa Sukari, Nairobi, hadi alipokata roho. Wanawake wamekuwa vyombo vya kuuawa na kuonekana kuwa viumbe dhaifu.

Ubabe dume umezidi.Pambazuko ilitembelea kituo cha Muhuri, ambao ni watetezi wa haki za binadamu hasa haki za wanawake na watoto, ili kuliulizia swala hili la mauaji na mateso kwa wanawake.

Tulikutana na Bw. Francis Auma [afisa wa Rapid Response] “ kwa miaka mingi sana wanawake wamepitia maovu ya kudhalilishwa na jamii kutokana na tamaduni zetu za kiafrika” akasema bwana Auma, “maswala mengi yanachangia wanawake kuwa katika hali ya unyonge mbele ya wanaume, umaskini ni chanzo cha kwanza kikubwa, mtu anaona heri nibakie hapa kwa mume wangu nivumilie matatizo ili niukwepe umaskini”. Aliendelea Bw.Auma.

Muhuri, imeanzisha miradi ya kuinua hadhi ya jinsia ya kike katika njia moja au nyingine. ‘Madam President program’ ni moja ya miradi ambayo imeanzishwa na Muhuri ili kuwasaidia wanawake.

Wanawake wowote wanaopitia hali ngumu ya kudhulumiwa na kudhalilishwa na waume zao ni bora wawasilishe kesi zao mapema ili kuepuka kufikia hatima za waliouawa kama marehemu Sharon Otieno na wenzake.

………………………………………………………

Je, kipindi cha “Madam President” kitasaidia?

Kulingana na shirika la Muhuri, kipindi kipya kabisa kinachoendelea hewani mwa runinga cha “Madam President Program” kwa lugha rahisi ya Kiswahili, “Mheshimiwa Mama Rais” ni kana kwamba kinakusudia kuangazia baadhi ya changamoto ya kuleta suluhu kwa miongoni mwa baadhi ya dhulma ambazo kina mama barani Afrika, Kenya ikiwemo zinawakabili kimaisha ya kila siku.

Kwanza kabisa tungetaka kushuhudia haki imetendeka hasa kwa mauaji ya dada wetu watatu ambayo yaliwashangaza wengi siyo hapa nchini Kenya tu bali inje ya nchi. Twataka kuona haki imefanyika kwa sheria kuwabana waliohusika na mauaji ya Sharon Otieno, Monica Nyawira Kimani na Mildred Odira.

La kuhuzunisha zaidi ni kisa cha mauaji ya Sharon Otieno ambaye licha ya kuangamizwa maisha yake, pia kijuza cha mtoto aliyekuwa naye tumboni hali kadhalika kilikatizwa maisha yake na mafidhuli wauaji ambao wanazidi kujivinjari na familia zao huku familia ya Sharon, hususan watoto wake na wazazi wakiwa wahuzunika kila kukicha.

Hali ni vivyo hivyo kwa washukiwa wa mauaji ya Monica Nyawira Kimani ambayo vile vile yamezingirwa na rangirangile ya kutofahamika jinsi haki inavyoendelea kufuatwa ili kutujuza la maana kuhusu hatua marudufu inayochukuliwa. Ni hali hiyo hiyo pia ya kizungumkuti tunachoshuhudia katika kesi ya mauaji ya hivi punde mwanzoni mwa mwaka huu ya Mildred Odira.

Katika mazingaombwe ya mauaji yote haya matatu na mpaka yale yaliyoripotiwa majuma machache yaliyopita, tumeona visa vya vihoja vya mauaji ya kufadhahisha. Utamuua vipi mwenzako sawia na jinsi unavyomfinyanga umbu ama nzi. Ulimwengu wa wanaume wetu umepasukia wapi ndio waone kuwa sisi wanawake ulimwenguni ndio kiumbe dhaifu?

Madam President

Ni wito wa wanawake wote kwamba jitihada zaidi zinahitaji kuhakikisha kwamba haki ya mwanamke imelindwa na kupatikana kwa wale waliodhulumiwa. Sheria na kanuni zake lazima zifuatwe na mila na utamaduni wetu pia kupigwa msasa haswa wakati tamaduni nyingine zinaonekana kuwafinyilia kina mama na kuwapendelea wanaume kwenye jamii zao.

Kipindi cha runinga cha “Madam President” kinawapa motisha wanawake chungu nzima ambao wameanza kutambua kwamba kila kazi ni bidii na fikra thabiti kufaulu. Wanawake wa mashambani nao wanastahili kuhamasishwa haki yao kwani tunayo Imani tele kwamba tangu mkutano wa haki ya kina mama wa Beijing miaka ya nyuma, kina mama barani afrika wamepiga hatua si haba.