Taarifa zote kuhusu ndege aina ya Boieng 737-8 Max zimenakiliwa kwa uchunguzi wa kimaabara

Shirika la Usalama na Uchunguzi wa Safari za Ndege, nchini Ufaransa limethibitisha kwamba taarifa zote kuhusu ndege aina ya Boieng 737-8 Max lililohusika kwenye ajali nchini Ethiopia, zimenakiliwa kwa uchunguzi wa kimaabara.

Kisanduku cheusi cha kuhifadhi mawasiliano, Black Box kilipatikana mnamo Machi 11 kisha kutumwa nchini Ufaransa kusaidia wachunguzi kubaini kiini cha ajali hiyo.

Waziri wa Uchukuzi nchini Ethiopia Feraj Fekeza aidha amedokeza kwamba pande zote zinazidi kushirikiana kufanikisha uchunguzi huo.

Mapema jana maelfu ya Raia wa Ethiopia walihudhuria hafla ya mazishi ya pamoja ya baadhi ya watu waliofariki dunia kufuatia ajali ya Ndege ya Ethiopian Airlines Jumapili iliyopita. Jamaa za waliofariki Ethiopia walibeba jeneza kumi na saba bila mili kwa maziko.

Ikumbukwe maafisa wa serikali ya Ethiopia Alhamisi wiki iliyopita walianza kukusanya chembechembe za msimbojeni yaani  DNA ili kuanza uchunguzi wa kuwasaidia jamaa kuwatambua wapendwa wao.

Related Topics