"Sina kinyongo na Ruto", Raila asisitiza

Na Caren Omae,

 

NAIROBI, KENYA, Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga amesisitiza kwamba ushirikiano baina yake na Rais Uhuru Kenyatta haulengi kumzuia Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

 

Akihojiwa wakati wa kipindi cha Point Blank katika runinga ya KTN News, Raila kwa mara nyingine ameyafutilia mbali madai kwamba, familia ya Kenyatta, Moi na Odinga zinapanga kushirikiana kuendelea kuliongoza taifa hili na kuwafungia nje Wakenya wengine.

 

Wakati uo huo, amesema ataendelea kushirikiana na Rais katika juhudi za kukabili ufisadi hasa miongoni mwa maafisa wakuu serikalini.

Kuhusu suala la kuifanyia katiba marekebisho, Raila amewakosoa wale wanaopinga pendekezo hilo akisema vipo vipengele katika katiba vinavyofaa kufanyiwa marekebisho kwa manufaa ya Wakenya.

 

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Afrika AU aidha ameunga mkono pendekezo la Tume ya Uchaguzi IEBC kubadilisha jinsi uchaguzi nchini unavyoendeshwa. Amesema kuwa shughuli ya kuwachagua viongozi sita kwa wakati mmoja kunawatatiza Wakenya.

 

Ikumbukwe wiki jana, alipokuwa akihutubu wakati wa kutolewa kwa ripoti ya uchaguzi wa rais mwaka wa 2017 Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alipendekeza uchaguzi kuendeshwa kwa awamu mbili tofauti, katika ngazi za kaunti na kitaifa ili kuhakikisha makamishna wanaendesha shughuli hiyo kwa njia ya uwazi.

Related Topics

Raila