Washukiwa wa ugaidi walivamia eneo la Shimbirey, Kaunti ya Garissa

Maafisa wa usalama usiku wa kuamkia leo wamefaulu kuwakabili washukiwa wa Kundi la Kigaidi la Al Shabaab walioivamia kambi ya wafanyakazi wa kampuni moja ya Uchina kwenye  eneo la Shimbirey Kaunti ya Garissa.

Inspketa Mkuu wa Polisi, Joseph Boinet amesema washukiwa walitoweka wakiwa na majeraha ya risasi. Awali wakazi wanaoishi karibu na kambi hiyo waliripoti kusikia mlio mkumbwa unaoaminika kuwa wa gruneti kisha kufuatia na milio ya risasi.

Hayo yanajiri huku polisi walitoa picha za washukiwa tisa wanaohusishwa na shambulio la kigaidi kwenye eneo la 14 Riverside Drive ambako watu 21 waliuliwa. Miongoni mwa washukiwa hao ni mwanamke kwa jina Violet Kemunto ambaye ni mke wa Ali Salim Gichunge, mmoja wa washukiwa waliolivamilia eneo hilo.

Washukiwa wengine ni Boru Abdi Bidu, Didu Mohamed Fugicha, Abdi Ali Kachora, Gaddafi kwa jina la utani Munene, Ramadham Wario Bonaya kwa jina la utani Rasho, mwingine kwa jina Omari na Hussein Adan Hussein kwa jina la utani Etto. Hata hivyo jina la mshukiwa mwingine halikuwa wazi japo polisi walitoa picha yake. Polisi wamesema washukiwa hao ni hatari kwani wamejihami hivyo kutoa wito kwa umma kuwa makini na kutoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwao.

Imebainika kuwa bunduki tatu miongoni mwa tano zilizotumiwa katika shambulio la 14 Riverside Drive ziliingizwa nchini kutoka Somalia na zinaaminika kuwa za jeshi la taifa hilo ambazo ziliibwa na washukiwa wa ugaidi. Kufikia sasa washukiwa takriban kumi wamekamatwa kwa kuhusishwa na shambulio hilo huku wengine 30 wakihojiwa. Miongoni mwa waliokamatwa na kuwasilishwa mahakamani wili iliyopita ni  washukiwa sita wakiwamo madereva wawili wa taxi na mhudumu wa duka la Mpesa wanaoaminika kuwasiliana na washukiwa wa shambulio hilo. Aidha mwingine aliyekamatwa ni babaye na mkewe mshukiwa kwa jina Mahar Khalid Riziki ambaye alinaswa katika Kamera za CCTV akijilipua nje ya Hoteli ya Dusits D2.

Related Topics

Garissa Al Shabaab