Mahakama imemwachilia huru Gavana Okoth bado

Mahakama ya Kibera memwachilia huru Gavana wa Migoro Okoth Obado kwa bondi ya shilingi laki tano na mdhamini wa kiasi sawa na hicho au thamana ya shilingi laki mbili pesa taslimu.

Akitoa uamuzi huo, hakimu Joyce  Gandani amefutilia mbali ombi lililowasilishwa na upande wa mashtaka ukitaka Obado aendelee kuzuiliwa kwa siku kumi na tano zaidi ili kuwapa nafasi kukamilisha uchunguzi. Katika uamuzi huo, Obado hata hivyo ameonywa dhidi ya kuwaingilia mashahidi.

Wakati uo huo mahakama imesema kwamba upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha kuonesha iwapo mshukiwa angeingilia uchunguzi kwa njia yeyote ile.

Baada ya uamuzi huo upande wa mashtaka umewasilisha ombi kuitaka mahakama kumshurutisha Obado kuripoti katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi DCI kila Ijumaa. Hata hivyo mawakili wa Obado wamelipinga ombi hilo, wakisema ni kinyume cha sheria. Wakiongozwa na Cliff Ombeta wamesema iwapo mahakama itaruhusu ombi hilo, itakuwa ikishirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma DPP na DCI katika uchunguzi.

Obado amekuwa akizuiliwa tangu siku ya Jumatano alipokamatwa baada ya bunduki nane kupatikana nyumbani kwake. Alishtakiwa kwa kuzimiliki bila kuwa na leseni.