Wataalam kuteuliwa kujiunga na vikosi vya polisi

Huduma katika Idara ya Polisi zinaendelea kupigwa jeki kufuatia mipango mipya ambayo imezinduziliwa leo hii.

Sasa Wakenya wataweza kupiga ripoti kuhusu ukosefu wa nidhamu miongoni mwa maafisa wa polisi kwa njia ya kielektroniki bila kujitambulisha. Katika mpango huo mpya, Mkenya yeyote anaweza kutuma ujumbe mfupi kwa nambari 40683 au kupiga simu kwa 0800721230, baada ya hapo atapewa kodi maalum ambapo anaweza kufuatilia malalamiko yake.

Ikumbukwe mashirika ya Kijamii yamekuwa yakishinikiza mpango huo, ili kuwahakikishia usalama wananchi wenye malalamiko dhidi ya polisi pia, kufanikisha uchunguzi ambao hauegemei upande wowote.

Wakati uo huo, Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Fred Matiang'i ametangaza kuwa katika kipindi kijacho cha kuwateua makurutu watakaojiunga na vikosi mbalimbali vya polisi, watazingatia wale waliohitimu na taaluma mbalimbali.

Ikumbukwe awali mpango wa kuwateua makurutu umekuwa ukiwalenga wale waliokamilisha masomo yao hadi kufikia shule za upili na kuifanya Mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha Nne, KCSE.

Aidha Matiang'i amesema mabadiliko katika idara hiyo ya polisi yatatekelezwa kwa mujibu wa maagizo yaliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta.

Ameyasema hayo mapema leo alipozindua ofisi za kitengo cha kushughulikia malalamiko katika wizara yake. Kitengo hicho kimehamishwa kutoka Jumba la Harambee hadi ofisi mpya eneo la Upper Hill ili kuboresha utendakazi.  

Related Topics

Polisi Vikosi