Uteuzi wa Jubilee wafanyika Nairobi

Na, Mate Tongola
Huku matokeo ya uteuzi wa Chama cha Jubilee Kaunti ya Nairobi yakitarajiwa, visa vya vurugu na madai ya udanganyifu vilishuhudiwa.
 Askofu Margaret Wanjiru anayewania ugavana alikamatwa na polisi baada ya kuzua vurugu katika kituo cha kupigia kura City Park. Kwa sasa anaendelea kuzuililiwa katika Kituo cha Polisi cha Parklands.
Mike Sonko anayewania wadhifa huo, alilalamikia kukosekana kwa majina ya baadhi ya wapigakura katika sajili, huku akiwashauri wafuasi wake kusalia watulivu akiwahakikishia kuwa ataibuka na ushindi.
Matamshi sawa na hayo yametolewa na mshindani wake, Peter Kenneth huku akitoa wito kwa usimamizi wa Chama cha Jubilee kuendesha shughuli hiyo kwa njia huru na ya haki.

Rachael Shebesh ambaye anatetea wadhifa wake wa Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Nairobi, amedai kuwa baadhi ya washindani wake wana njama ya kumwangamiza.
Kwa upande wake, mgombea useneta Kaunti ya Nairobi, Johnson Sakaja ameeleza matumaini makubwa ya kushinda, huku akisema yu tayari kukubali matokeo ya uteuzi unaoendelea, iwapo atashindwa.
Sakaja anamenyana na Yvonne Khamati na Mutinda Kavemba.