Mgombea wa NASA asubiriwa kwa hamu

Na Caren Omae
Zikiwa zimesalia saa chache tu kabla ya muungano wa NASA kutangaza ni nani miongoni mwa vinara wake atakayepeperusha bendera ya muungano huo wakati wa uchaguzi mkuu ujao, maandalizi yamekamilika.
Macho yote sasa yameelekezwa kwa mkutano wa kesho ambapo itabainika ni nani miongoni Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Moses Wetangula na Musalia Mudavadi atakayewania urais.
Kamati andalizi ikiongozwa na Mbunge wa Tongaren, Eseli Simiyu imesema mkutano huo utahudhuriwa na vigogo wote wa NASA akiwamo Gavana wa Bomet, Isaac Ruto.
Gavana Ruto alijiunga rasmi na Muungano huo wiki jana wakati wa hafla iliyoandaliwa katika ukumbi wa Bomas.
Ikumbukwe tangazo litakalotolewa kesho linafuatia mazungumzo miongoni mwa vinara wenyewe baada ya kamati maalumu iliyoteuliwa kumchagua mmoja wao kukosa kuafikiana.