IEBC yasema wananchi watapewa fursa kubainisha iwapo wamesajiliwa kuwa wapigakura

Na, Mike Nyagwoka/Beatrice Maganga
Wakenya wametakiwa kutokuwa na hofu kuhusu sajili ya wapiga kura licha ya makosa madogo yanayoendelea kuibuliwa kwani  itafanyiwa ukaguzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Tume ya uchaguzi IEBC vilevile  imekana taarifa kuwa  kuna raia wa kigeni wanaosajiliwa kuwa wapiga kura nchini.
Katika kikao na wanahabari, Tume ya Uchaguzi IEBC imesema watu alfu mia moja ishirini na wanane, mia tisa ishirini na sita miongoni mwa waliosajiliwa wana nambari za vitambulisho vya kitaifa zinazolingana na za wengine. Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati hata hivyo amesema dosari zilizipo zinashughulikiwa.
Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Ezra Chiloba amesema pindi usajili wa wapigakura utakapokamilika,  waliosajiliwa watapewa fursa ya kubainisha iwapo wamesajiliwa kwa kutumia nambari ya simu ama kwa kuzuru ofisi za IEBC, shughuli itakayoendelea hadi wakati wa uchaguzi. Aidha  kwa mujibu wa sheria kunatarajiwa  kuandaliwa shughuli  rasmi ya ukaguzi takriban miezi miwili kabla ya uchaguzi.
Wakati uo huo, IEBC imekana madai ya kinara wa CORD Raila Odinga ya kuwapo kwa  usajili wa raia wa kigeni. Hata hivyo, Chebukati ameahidi kuwa  iwapo watapokea taarifa hiyo rasmi, uchunguzi utaanzishwa na hatua za kisheria kuchukuliwa.
Na kuhusu madai mengine kuhusu uhamisho  wa wapiga kura yakiibuliwa, IEBC imesema haina msingi wowote wa kisheria kuzuia hilo kufanyika  kinyume na hapo awali ambapo sheria iliwaruhusu watu ambao wamekaa eneo kwa zaidi ya miezi sita kusajiliwa kwenye eneo hilo pekee wala si watu ambao hawajakaa eneo hilo kwa kipindi hicho.
Licha ya kutaja ukame kuwa mojawapo ya sababu zinazowafanya wakazi kwenye maeneo mengine kutojitokeza kusajiliwa kuwa wapigakura, Wafula na Chebukati wamewarai wananchi kusajiliwa.

 

Related Topics