Na Maganga
Wananchi wametakiwa kutahadhari kufuatia uwezekano wa kushuhudiwa kwa mashambulizi ya kigaidi wakati wa sherehe za krismasi na mwaka mpya. Idara ya usalama nchini imesema kwamba wanampango wa Al Shabaab na wale wa kundi la IS wanapanga kuyashambulia maeneo ya mpakani, Kaunti ya Mombasa vilevile magari ya uchukuzi wa umma.
Kulingana na Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet, Kundi la IS limekuwa likiendeleza usajili wa vijana nchini kwa lengo la kuwatumia kutekeleza mashambulizi. Katika taarifa, Boinett amesema kundi la Al Shabaab kwa upande wake limekuwa likijigawanya kwa vikundi na kupenyeza maeneo ya Mandera, Wajiri, Garissa na Lamu.
Amesema washukiwa wa kundi hilo wamekuwa wakitumia fursa ya mvua inayonyesha kuingia nchini hasa maeneo ya Kolbio Kaunti ya Garissa. Vilevile baadhi ya washukiwa wamekuwa wakidai kuwa wafugaji na kutafuta fursa ya kuingia nchini kutoka Somalia huku wengine wakitaka kuingia kupitia msitu wa Boni. Hata hivyo amesema usalama umeimarishwa katika maeneo yanayolengwa na magaidi.
Onyo hilo limejiri wakati ambapo mafisa wa kukabili ghasia pamoja na wenzao wa kitengo cha RDU wamenusurika kifo baada ya kilipuzi kilichotegwa ardhini kulipuka katika barabara ya Elwak-Dabacity, kaunti ya Mandera.