Wabunge wa Muranga waunga mkono mradi wa maji huku wanaharakati wakitaka usitishwe

Na Suleiman Yeri
Wabunge wa Kaunti ya Murang'a wameunga mkono mradi wa ukusanyaji na usambazaji maji ulio kwenye kauti hiyo kwa sharti kuwa ni lazima maeneo bunge yote yapate maji kupitia mradi huo.
Wabunge hao wametoa uamuzi huo baada ya kufanya mkutano na Waziri wa Maji, Eugene Wamalwa ulioandaliwa Jumatatu jijini Nairobi.
Huku hayo yakijiri wanaharakati wawili wameelekea mahakamani kutaka agizo la kusitisha mradi huo.
Wawili hao Okiya Omtatah na Florence Kanyua wameishtaki Bodi ya Huduma za Maji ya Athi na maafisa wengine wakuu kwa kutoa zabuni kisiri kwa kampuni ya China State Corporation kuendeleza mradi huo.
Wanaharakati hao wanadai kuwa zabuni hiyo ilitolewa kinyume na sheria na kandarasi ya mradi huo inayostahili kuanza wiki ijayo ilitiwa saini kisiri.
Hata hivyo Jaji wa Mahakma Kuu Joseph Onguto ametaka wote waliotjwa kwenye malalamishi hayo kufika mahakamani tarehe 26 mwezi huu kwa maelekezo zaidi. Jaji Onguto aidha amewataka wanaharakati hao kuwasilisha nakala zaidi kuimarisha ushahidi wao.