Serikali kutwaa silaha kutoka kwa wananchi Kerio Valley

Na Carren Omae

Kufuatia ghasia ambazo zimeendelea shushuhudiwa kati ya jamii za Pokot na Marakwet eneo la Kerio Valley, serikali imeendelea kuweka mikakati ili kurejesha utulivu eneo hilo. Mbali na maafisa wakuu kuhamishwa, serikali imetangaza kuanza oparesheni ya kuzitwaa kwa lazima bunduki zinazomilikiwa kinyume na sheria kutoka kwa wenyeji.

Wakati wa mkutano ulioongozwa na Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi, Joel Kitili na Kamishna wa eneo la Bonde la Ufa, Wanyama Musiambo maafisa wa usalama eneo hilo wameagizwa kuwakabili vilivyo wakazi wanaomiliki bunduki kinyume na sheria. Kamishna huyo amesema serikali itaendeleza shughuli hiyo hadi itakapohakikisha hakuna mkazi anayemiliki bunduki.

Akizungumza baada kuzuru maeneo ya Tot na Soko Bora Marakwet Mashariki, yaliyoathirika zaidi na wizi wa mifugo, Musiambo aidha ametaja umiliki wa silaha kuwa chanzo cha ongezeko la wizi wa mifugo na mauaji ambayo yameshuhudiwa eneo hilo.

Wakati uo huo amesema maafisa wa usalama wanawasaka washukiwa wa wizi wa mifugo ambao tayari wanajulikana. Aidha ameongeza kuwa maafisa zaidi wa akiba watatumwa katika maeneo yaliyoathirika kuimarisha usalama huku akiahidi kwamba mifugo yote iliyoibwa itarejeshwa.
Katika kipindi cha wiki moja pekee watu kumi na watano wameuliwa na mamia ya wengine kuachwa bila makao kufuatia visa hivyo.