Haifai kuwahangaisha magavana mara kwa mara asema Naibu wa Rais

Na Beatrice Maganga
Naibu wa Rais William Ruto amelalamikia hatua ya mabunge ya kaunti kupitisha mara kwa mara hoja ya kuwabandua ofisini magavana. Ruto amesema madai yanayoibuliwa dhidi ya magavana na wafanyakazi wengine wa kaunti yanastahili kuwa na msingi, badala ya kulenga kuwaharibia sifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Ugavi wa Mapato, CRA Micah Cheserem amesema utendakazi kwenye kaunti umeathiriwa kwa kiasi kikubwa na malumbano baina ya wawakilishi wa wadi na magavana.
Walikuwa wakizungumza wakati wa mkutano ulioandaliwa katika ofisi ya Naibu wa Rais jijini Nairobi, uliowaleta pamoja magavana, wawakilishi wa Wizara ya Fedha miongoni mwa wengine kujadili masuala mbalimbali kuzihusu kaunti.
Hayo yakijiri, licha ya Gavana wa Nyeri Nderitu Gachagua kuondolewa shutma dhidi yake baada ya awali bunge la kaunti hiyo kuidhinisha hoja ya kumbandua ofisini kwa misingi ya kushiriki ufisadi miongoni mwa madai mengine, baadhi ya wawakilishi wa bunge hilo sasa wanapendekeza ashtakiwe mahakamani. Wanasema kuhukumiwa kwa watu watatu waliokuwa maafisa wa kaunti baada ya kupatikana na hatia ya ukiukaji wa sheria za ununuzi ni dhihirisho tosha kwamba kuna makosa makubwa ambayo yamekuwa yakifanyika kwenye kaunti hiyo.
Watatu hao ambao ni aliyekuwa afisa wa ardhi John Mwangi, Martin Wamwea wa Fedha na aliyekuwa Afisa wa Utumishi, Simon Wachira walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela wiki hii, la sivyo walipe faini ya shilingi milioni ishirini na nne baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka sheria za ununuzi.
Hata hivyo waliwasilisha rufaa leo kupitia Wakili Edward Oonge kupinga uamuzi huo. Rufaa hiyo itasikilizwa Oktoba 17.