Mdudu mtu, tafadhali badilika!

Kwa kweli umbo lake halieleweki na linaashiria haswa matendo yake.Mara nyingi hana haraka wala kelele na anapoamua kutekeleza uhuni wake habahatishi. Hata hivyo, anajitia kulifahamu shamba na utamu wa nafaka kuliko mkulima mwenyewe.

Licha ya hayo, yeye hula bila kujua ni nani aliyetengeneza au kupanda. Vile vile hula kwa dharau akiharibu bila kujali juhudi zilizotumika kutengeneza chambilecho wahenga 'ukiona vyaelea vimeundwa’.

Naam, machozi, damu na mahangaiko ya mwenye kupanda hayamtishi maanake yuko kwenye chungu na funguo zote. Ni jambo la huzuni sana kwa sababu hizi ndizo sifa za viongozi fisadi wasio na hisia hata chembe. Jamani mbadilike.