Rais Kagame: ubwanyenye ni matokeo ya kuwa madarakani kwa muda mrefu sana

Dhamira ya Rais Paul Kagame kutaka kujipatia muhula wa tatu haueleweki. Ameonekana kwa miaka mingi sasa kama rais aliyeitoa nchi yake kutoka safisha safisha za kikabila hadi kuwa nchi tulivu na yenye ustawi. Shida ni kwamba mara kwa mara, kuna ukandamizaji wa upinzani. Kwa jumla, ni kiongozi mzuri. Sasa anaonekana amelewa na madaraka na hataki kutoka usukani. Haya ndiyo maneno yanayoirudisha Afrika nyuma.

Kote Afrika Kati iwe DRC, Burundi au sasa Rwanda, viongozi wanataka kukalia madaraka kwa muda usiokubalika kikatiba. Chanzo chao cha kutaka kuendelea kwenye uongozi ni kukandamiza upinzani na pia kufurahisha vibaraka wanaowapotosha kuendeleza mihula yao ya uongozi.

Rwanda ni nchi nyeti hususan ukikumbuka ya kwamba ni miaka ishirini nyuma tu nchi hiyo ilipokuwa kwa michafuko ya kikabila. La muhimu ni kuwa viongozi wa kiafrika kuheshimu katiba na kuelewa ya kwamba sauti ya wananchi lazima isikike. Kutisha na kufurusha upinzani huzorota taifa na kudhofisha misingi ya kidemokrasia. Inabidi Rais Kagame atoke madarakani awachie Wanyarwanda  wachague mtu tofauti kuongoza nchi yao.