Jameni, tuwaheshimu hawa mashujaa wetu

Leo hii tunasherehekea mashujaa waliopigania uhuru wa nchi yetu Kenya. Mashujaa ambao walijitoa kihali na mali kuhakikisha kwamba tunajitawala kivyetu vile tupendavyo. Japokuwa matamanio ya wazee hawa yaweza kuwa hayajaafikiwa mia fil mia, ni vyema kuwapongeza kwa kazi yao shwari.

Kazi yao ilitufanya kuabiri magari sawa na watu wa matabaka tofauti tofauti na hata watu wa rangi mbali mbali bila kuwazia atokako mtu. Yaani kwa ushujaa wao wa kukubali kuishi msituni kulikokuwa na hatari mbali mbali kama vile wanyama pori na baridi kali ya kufanya mtu azizime.

Walistahimili yote haya, hasa kujinyima starehe zao za kibinafsi walizopata walikokuwa wanaishi ili nchi hii tukufu ipate fursa ya kujitawala. Wazee hawa, ambao wakati huo walikuwa wenye nguvu na jazba ya kujitawala, walitutendea mema ambayo hatuwezi kulipa kiholela.

Japokuwa mateso waliyopitia miaka kabla ya 1963 yanaendelea kutaniwa na vijana wasiojua kilichoendelea, ni swala la kutamausha sana. Naishi kuamini kwamba hakuna kitu kinachofaa kudhaminiwa na kuheshimiwa kama ile hali ya mtu kuwa tayari kuaga dunia akitetea nchi yake. Mtu akikubali kwamba ataiondokea familia yake ili ahakikishe kwamba vizazi vijavyo vitaishi raha mstarehe bila kuagizwa kubeba vipande wanapozuru maeneo fulani nchini mwao.

Mtu anayejitoa mhanga kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo vitaishi kwa amani na watapanda mimea, kufuga wanyama na watasomea shule wazitakazo bila kubaguliwa kutokana na rangi ya ngozi yao. Kwa mukhtasari, nimeishi kuamini kwamba wazee hawa mashujaa walishika dini sana kiasi ya kwamba walimuiga Yesu Kristo. Wakataka kufanana naye.

Wakakubali kuuawa huko msituni wakipigania vizazi ambavyo walikuwa na matumaini navyo.  Kusema kweli, watu hawa walitufaa pakubwa. Wanafaa kuheshimiwa na sanamu zilizopo mijini Nairobi na Machakos ya mashujaa inadhihirisha kazi bora waliofanya. Tukiendelea kuwasherehekea mashujaa wetu kumezuka kizazi ambacho hakisikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Kizazi kisichojali kuhusu jana wala leo, itakuwa kesho?

Kizazi ambacho kinachochezea uhuru uliopatwa kupitia umwagikaji wa damu isiyonahatia wakati ule hali ilipokuwa ngumu sana. Kizazi ambacho kwa kuchukua simu na kurekodi video wanapotusi mawaziri serikalini ndio njia faaufu kueleza matatizo yanayowakumba.

Da! Tabia za kupotosha na za kuaibisha kwa kizazi hiki kinachotumia mitandao kwa tabia mbaya ya aina hii. Mitandao hii vile vile, inaendelea kutumika kuwaharibu vijana hawa kutokana na ongezeko la visa vilivyoripotiwa. Wapo vijana tele walionaswa wakitazama filamu za anasa kwenye maeneo ya kuonyesha filamu.

Hivyo basi, kupitia visa hivi vinavyoweza kuwashtua mashujaa wetu walioaga miaka ya awali ni sharti kizazi kilicho na umri wa makamu kuhakikisha kwamba wanaonyesha hawa wadogo njia ya kufuata. Bila kufanya hivi tutakuwa na vijana wasiojua hayati Mzee Jomo Kenyatta,  Jaramogi Odinga, Tom Mboya na hata Dedan Kimathi waliifanyia nini nchi hii.

Itakuwa jukumu la kizazi hiki cha makamu kuhakikisha kwamba vijana wanatambua kwamba kuna maelfu ya watu waliojitolea kuhakikisha kwamba wanapata fursa ya kutumia mitandao bila uoga. Vile vile, kizazi hiki kichanga kitakapo zeeka kitanafasika kuwahadithia wale watakao kuwa wadogo wao ili nao wakaelewe pale nchi hii ilipotoka na inapoelekea.

Kizazi cha makamu au kwa wepesi tunaweza waita wazazi wamefeli kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata mafunzo kuhusu misingi ya nchi hii. Wamekosa kabisa kuwapa mafunzo ya kuwaelekeza watoto wao ili wasijihusishe na mambo ambayo hayatawaletea aibu wao pekee bali nchi nzima.

Watoto hawa wanakua bila kufahamu kuhusu mambo wanayohitajika kufanya kuhakikisha kwamba nchi inasonga mbele. Bila kuwaza sana kuhusu jinsi mashujaa wetu wanavyodhihakiwa na vijana hawa mbu mbu mbu wasiojua mbele wala nyuma, nina matumaini kwamba kesho yetu kama nchi itakuwa chanya.