;
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa hadi visa vinne kati ya kumi vya saratani duniani vinaweza kuzuilika iwapo sababu kuu za hatari zitadhibitiwa.
Uchambuzi mpya wa shirika hilo unaonesha kuwa takriban asilimia 37 ya visa vipya vya saratani vilivyoripotiwa mwaka 2022, sawa na visa milioni 7.1, vilihusishwa na sababu zinazoweza kuzuilika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa kwa kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani leo, matumizi ya tumbaku yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha saratani kinachoweza kuzuilika, kikichangia asilimia 15 ya visa vipya.
Maambukizi yanayosababisha saratani yanachangia asilimia 10, huku matumizi ya pombe yakihusishwa na asilimia tatu ya visa hivyo.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa saratani ya mapafu, tumbo na mlango wa kizazi huchangia karibu nusu ya visa vyote vya saratani vinavyoweza kuzuilika.
Saratani ya mapafu inahusishwa zaidi na uvutaji sigara pamoja na uchafuzi wa hewa.
Saratani ya tumbo inahusishwa kwa kiwango kikubwa na maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori, wakati saratani ya mlango wa kizazi husababishwa zaidi na virusi vya papilloma vya binadamu (HPV).
Utafiti huo pia umebaini kuwa wanaume wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani zinazoweza kuzuilika ikilinganishwa na wanawake.
Takriban asilimia 45 ya visa vipya vya saratani kwa wanaume vinahusishwa na sababu zinazoweza kuzuilika, huku kwa wanawake ikiwa ni asilimia 30.
Kwa wanaume, uvutaji sigara umetajwa kuwa sababu kuu ya hatari, wakati kwa wanawake maambukizi ndiyo chanzo kikubwa.
Tofauti za kijiografia pia zimeonekana katika mzigo wa saratani zinazoweza kuzuilika. Kwa wanawake, kiwango cha visa hivyo ni asilimia 24 katika Afrika Kaskazini na Asia Magharibi, huku kikifikia asilimia 38 katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa wanaume, Asia Mashariki inaongoza kwa asilimia 57 ya visa vinavyoweza kuzuilika, wakati Amerika Kusini na Karibea zina kiwango cha chini zaidi cha asilimia 28.
WHO inaonya kuwa saratani bado ni changamoto kubwa ya afya duniani, ikiwa ilisababisha vifo vya takriban watu milioni 10 mwaka 2020, sawa na kifo kimoja kati ya sita duniani kote.
Shirika hilo linaonya kuwa ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa, visa vipya vya saratani vinaweza kuongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2040.
Wataalamu wa afya wanasisitiza umuhimu wa hatua za kinga, zikiwemo udhibiti mkali wa matumizi ya tumbaku na pombe, utoaji wa chanjo dhidi ya HPV na homa ya ini aina ya B, kuboresha ubora wa hewa, kuhakikisha mazingira salama ya kazi, pamoja na kuhamasisha lishe bora na mazoezi ya mwili.