Kuna dalili za Kalonzo kuwa nyapara wa ikulu

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoki katika mahojiano na wanahabari wa the Standard katika nyumbani mwake Karen,Nairobi [Picha: Elvis Ogina.Standard]

Kalonzo Musyoka ataendelea kufuta madirisha na milango ya siasa nchini hadi atakapoacha kushiba na mkoa mashariki alikozaliwa na kuanza kuchangamkia kura na radhi bwerere za magharibi na mwambao wa Kenya – jambo ambalo halitatokea kwenye uhai wa Jamhuri hii labda paka azae na kunguru.

Kwa pimo la mukabala tuelekeapo 2022 na kima cha historia fiche tangu NARC ikomeshe himaya ya KANU, ni rahisi kutafsiri chupa kuliko sufuria unapokumbuka na jinsi hii ya mpika -  maoni aliyekubuhu Janjaure za ndumakuwili na zile za Jogooo la shambani kuwika mjini. Kwa ugumu wa kongoreti wakumuelewa na kumueka fungu sokoni, itabidi masabasi wao pandashika za vyama vingi vya siasa nchini Kenya wakubaliane na mimi kwa moja: kwa

katibu huyo mwandazi wa KANU enzi za Raisi Dainiel Arap Moi aliyehudumu muda mrefu (1988 – 2004) na mbunge wa zamani wa Kitui Kaskazini (1985 – 1997) na pia Mwingi Kaskazini (1997 – 2013), kitu ujanja wa siasa usioeleweka guu wala kichwa ni jambo la kawaida kwake.

Amekuwa mzoefu serikalini hivyo ana weledi wakuzama baharini na wenzake na kuibuka salama salimini huku wenzake wakifa maji ama kufilia mbali bila kupata muokozi. Wengi wao walioogelea ufuoni wamembaandika majina mengi mfano “Msaliti”  “Kigeugeu” “tikiti – maji” na hata “Kunguru muoga” Kalonzo ameshangaza wengi kwa kuweza kuwa waziri mwenye nyadhifa enzi za maraisi wawilli (Moi na Kibaki) waliofurusha waitifaki wengi wenye tajiriba kubwa kushinda yeye.

Mwana huyu wa ukambani anafahamu tangu enzi hizo namna ya kuingia katikati ya meno ya mamba ama kidami cha simba na kutoka bila mikwaruzo wala jeraha lolote. Kwa sasa tangu azibuke shimoni baada ya uchaguzi mkuu tata uliopita wa 2017 nakufanikiwa kuitwa serikalini chini ya kivuli cha raisi Uhuru na Raila, amerudi kwa kishindo naku

pewa wadhifa mkubwa kama mwandani wake wa NASA Raila Odinga. Tatizo ni kuwa hasongi kuwa Raisi wa Jamuhuri hii na amekuwa nyapara wa ikulu. Huenda makamu wa raisi huyu akawa anafahamu vyema sauti na harufu yake (ikiwemo chama chake cha wiper) ni sumu baridi Nyanza, Bonde la Ufa na mkoa wa kati ambapo jamii za waluo, wakalenjin  na wakikuyu wana watakatifu wao wa nyuimbani walengwao  kutawala nchi hii moja baada ya mwingine kwa ufupi, Kalonzo hana chake miongoni mwa wateule kwenye idadi, migodi, majadi na jadi adhimu kileleni.

Stephen Kalonzo Musyoka mwenye umri wa miaka 65 amezliwa Tseikuru Disemba 25, 1953 enzi za mkoloni mwingereza na anakumbukwa kama mwanasheria kigogo aliyeweza kuingia siasa na kuhudumu kama makamu Raisi wa kumi wa Kenya kuanzia 2008 hadi 2013. Alikuwa waziri wa mambo ya kigeni 1993 hadi 1998 kisha enzi za Kibaki akahudumu wadhifa huo huo 2003 hadi 2004 kabla kuteuliwa waziri wa mazingira 2004 hadi 2005. Alishindwa kama mgombea Uraisi 2007 lakini akateuliwa makamu Raisi

mnamo 2008 baada ya Raila kutofautiana na Mwai Kibaki. Ameitwa “tigiti – maji” asiyeeleweka atakako na aendako. Tigiti - maji ni tunda ambalo kwa nje ni rangi ya kijani lakini ndani ni jekundu. Nakumbuka 2010 kura ya maoni Agosti 4 kuchagua mwongozo wa katiba mpya ambapo, “Timu ya Kijani” iliunga mkono ilhali “Timu manjano” ilipinga mchakato huo. Kalonzo alivaa fulana ya manjano lakini wengi walimshuku mbabe huyo anasaidia timu pinzani kisirisiri uwanjani mpaka wa leo ni wachache wanaomuamini ama kumuenzi. Kule ukambani, Magavana Dkt. Alfred Mutua (Machakos) Charity Ngilu (Nyeri) na professa Kivuitha Kibwana hawamthamini na hasa Dkt.

Mutua anaezongwa na rundo la wawakilishi kaunti (MCA) wa Wiper Democratic Movement (WDM) wanaoongozwa na kiongozi wa wengi bungeni Mark Muendo. Charity Ngilu hana haja naye tangu enzi za Pentagon chini ya Raila na ametuhumu kuingililia siasa za Kitui na kumchimba. Swali linakuja: Kwa nini Kalonzo hataki Uraisi ilhali ametamba sana kimataifa na kaitaifa? Je, ni uwoga ama usungura wa mtegemea – nundu – haachi – kunona? Kivipi amemea mbawa za kunguru na kukubali kufanya kiraka na tambara bovu na Maraisi wote watatu waliotawala Kenya baada Jomo Kenyatta?

 Mpaka lini ategemea kuvuna asichokipanda? Ama ni historia katara ya jamii yake ya ukambani (iliyoanza enzi za wafanya biashara wa kiarabu) waliokuwa wakisafirisha bidhaa  baina ya Pwani na falme ya Buganda, wagikuyu na kabila zengine za Bara Kenya? Je Kalonzo amerithi uhamali na ugawadi wa enzi hizo? Katika historia ya Kenya huru, Kalonzo amejenga kumbukumbu ya kuwa mwepesi kuingia upinzani mambo yakimuharibikia serikalini kuliko viongozi wa mikoa mengine ya Kenya. Hata hivyo, kutamani uraisi si dhambi wala tusi la nguoni lakini kwa Kalonzo vikwazo vya msingi nje ya uwezo wake na vyenginevyo vya kujitakia haviruhusu kutimiza tamaa hiyo.