Mama wa mwanamuziki wa nyimbo za njili nchini Betty Bayo, amewasilisha rasmi ombi kwa Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma nchini (ODPP) ili kufunguliwa uchunguzi rasmi kuhusu kifo cha binti yake.
Katika barua iliyotolewa Desemba 9, 2025, na kuwasilishwa kupitia wakili wake, Joyce Wairimu, mama huyo aliomba DPP kuingilia kati, akisema familia imebaki na maswali ambayo hayana majibu na wasiwasi unaoongezeka kuhusu hali halisi iliyosababisha kifo cha msichana huyo.
Ombi hili linachukua hatua ya kisheria ya kwanza ya familia katika kujaribu kupata uchunguzi wa kina kuhusu siku za mwisho za Bayo kabla ya kifo chake pamoja na hatua zilizochukuliwa baada ya hapo.
Kulingana na ombi hilo, familia inadai kuwa Bayo hakuwa na ugonjwa wowote unaojulikana wakati wa kifo chake na kwamba kifo chake kilitokea ghafla.
“Familia imekabiliwa na maumivu yasiyovumilika katika kukubali ukweli kwamba marehemu, ambaye hakuwahi kuwa na ugonjwa wowote, angefariki kwa namna isiyoelezeka,” barua hiyo inasoma.
Wairimu anasisitiza kwamba kutokuwepo kwa rekodi za matibabu zinazoonesha hali ya afya ya awali ya mwanawe kunachochea shaka zao. Familia pia inadai kwamba hawakupata ripoti ya uchunguzi wa maiti (autopsy) au nyaraka zozote za matibabu zinazohusiana na hali ya afya ambayo Bayo alidaiwa kutibiwa kabla ya kifo chake.
Wanasisitiza kwamba ukosefu wa rekodi rasmi za matibabu umefanya iwe vigumu kuelewa kilichotokea na kama taratibu zote za kisheria na kiafya zilizingatiwa kikamilifu.
Mintarafu ya hayo, maombi hayo yanaonesha kuwa familia haikuwa na kuridhishwa na kile walichokiita haraka isiyo ya kawaida ya maandalizi ya mazishi.
Wairimu anabainisha kwamba kasi ya maandalizi hayo, pamoja na kutokuwepo kwa matokeo ya uchunguzi wa maiti, imechochea imani yao kwamba maelezo muhimu yanaweza kuwa yamepuuziwa au kufichwa.
Kwa kuzingatia wasiwasi huu, Wairimu anaomba DPP iandike barua kwa Kamishna Mkuu wa Polisi ili kudhibiti haraka suala hili na kufunguliwa uchunguzi wa wazi.
Mwanamuziki huyo wa Injili, anayejulikana zaidi kwa wimbo wake maarufu “11th Hour”, anadaiwa kufariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.
Habari za kifo chake zilithibitishwa na mpenzi wake wa zamani, Askofu Victor Kanyari.
Bayo anadaiwa kupumua mara ya mwisho karibu saa 7 mchana Jumatatu, Novemba 10, 2025.
Stay informed. Subscribe to our newsletter