×
App Icon
The Standard e-Paper
Kenya's Bold Newspaper
★★★★ - on Play Store
Download Now

Nyaribo aponea chupuchupu baada ya kuokolewa na Bunge la Seneti

Gavaana wa Nyamira Amos Nyaribo akipiga simu wakati wa mjadala wa kungatuliwa kwake mamlakani katika Bunge la Seneti Desemba 3, 2025. [Boniface Okendo, Standard

Gavana wa Nyamira, Amos Nyaribo, ameponea jaribio la kung’olewa mamlakani baada ya kuokolewa na Bunge la Seneti.

Siku ya Jumatano Bunge hilo la Seneti lilibaini ya kuwa Bunge la Kaunti halikufuata taratibu zinazohitajika kisheria ili kumngatua Nyaribo.

Nyaribo aliishawishi Seneti kwanza, ijadili na ipigie kura pingamizi ya hoja yake ya awali (Preliminary Objection) alilowasilisha, akisema kuwa Bunge la Kaunti halikufikia kiwango cha kisheria kinachohitajika ili kumng’oa ofisini.


Jumla ya maseneta 38 walipigia kura kuunga mkono hoja hiyo, na hivyo kumpa nafasi ya kuepuka kusikilizwa kwa mashtaka kamili, baada ya kubainika kuwa Wawakilishi Wadi walikiuka sheria katika kura yao.

“Maseneta usiku wa leo wamepiga kura kuunga hoja ya ililowasilishwa na Gavana Amos Nyaribo wa Kaunti ya Nyamira, kupinga kusikilizwa kwa mashtaka yake ya kutimuliwa, kwa msingi kwamba Bunge la Kaunti halikufikia kiwango kinachohitajika wakati wa kupiga kura. Hivyo basi, mchakato wa kumwondoa madarakani unakoma na Gavana Nyaribo atasalia ofisini,” alisema Spika wa Seneti Amason Kingi mara baada ya matokeo kutangazwa.

Kiini cha pingamizi hiyo kilikuwa ni ufafanuzi wa kile kinachounda "kizingiti cha kura" katika Bunge la Kaunti, na iwapo sheria inaruhusu Wawakilishi Wadi kupiga kura kwa uwakilishi (proxy voting).

Katika kikao chake cha Novemba 25, Bunge la Kaunti ya Nyamira lilikuwa na MCAs 19 pekee waliokuwepo ndani ya ukumbi, lakini kura 23 zilihesabiwa kupitisha hoja ya kumfikisha gavana Senetini.

Spika Thadeus Nyabaro, alipuuzia Kanuni nambari 67 ya Kanuni za Bunge la Kaunti ya Nyamira, inayotaka maamuzi yote yafanywe na “wanachama waliopo kwa kupiga kura.”

Badala yake, akatumia Kanuni ya Kudumu nambari 1 inayomruhusu kutoa mwongozo pale ambapo kanuni hazitoi maelekezo ya kutosha.

Kwa kufanya hivyo, Nyabaro aliwaruhusu Wawakilishi Wadi wanne ambao hawakuhudhuria kupiga kura kwa njia ya uwakilishi, hali iliyompa Nyaribo msingi wa kuhoji uhalali wa kura hizo, hasa baada ya Wawakilishi Wadi watatu kati ya hao wanne kukana kutoa idhini ya maandishi kumruhusu spika kuwateua wapiga kura wao mbadala.

Mbali na suala la kura kwa uwakilishi, Seneti pia ilipaswa kuamua iwapo Bunge lilifikia kizingiti cha thuluthi mbili kinachohitajika ili hoja ya kumwondoa gavana iweze kupita.

Wakili wa Bunge la Kaunti, Katwa Kigen, alidai kuwa kiwango cha thuluthi mbili hutegemea idadi halisi ya wajumbe waliopo wakati huo, na hivyo kinaweza kubadilika iwapo kuna nafasi zilizo wazi.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 33(2) cha Sheria ya Serikali za Kaunti, “wanachama wote wa bunge la kaunti” wanapaswa kupiga kura.

Hata hivyo, wakati wa kuwasilishwa kwa hoja hiyo, Bunge lilikuwa na wanachama 32 pekee kati ya 35, baada ya wadi tatu kuwa na chaguzi ndogo..

Hii ina maana kuwa kiwango cha thuluthi mbili kilipaswa kuwa 24 na siyo 23; kisheria thuluthi mbili ni sawa na kura 23.33, na hivyo ni lazima ziwe angalau 24.

“Tumealikwa ipasavyo, au gavana ameletwa kupitia mlango, ama suala hili limetupwa kupitia dirishani?” alihoji Kiongozi wa Wengi katika Senetini, Aaron Cheruiyot, akiunga mkono kura ya kuamua pingamizi hilo.

“Kanuni ya msingi ya Kifungu cha 33 haijatekelezwa,” akasisitiza Seneta wa Nandi, Samson Cherargei.

Madiwani Priscilla Nyatichi, Julius Obonyo, Elijah Abere, na Gladys Moraa walitarajiwa kutoa ushahidi endapo kesi ingefika kwenye usikilizaji kamili, baada ya wao kukanusha barua zilizotumwa kwa Spika wa Nyamira zikidai kuwa waliidhinisha wapige kura kwa niaba yao.