Watu 18 akiwamo Meya wa Kusini mwa Mexico wameaga dunia

Shambulio limetokea kwenye Jimbo la Guerrero, Mexico [Istock]

Watu kumi na wanane akiwamo Meya wa Kusini mwa Mexico wameaga dunia nchini Mexico kufuatia shambulio lililotekelezwa na watu wasiojulikana.

Kulingana na Televisheni ya Milenio nchini humo, shambulio hilo limetekelezwa katika Eneo la San Miguel Totolapan kwenye Jimbo la Guerrero.

Katika shambulio hilo watu wawili wamejeruhiwa vibaya.

Inaaminika kwamba shambulio hilo limetekelezwa na wanachama wa kundi la walanguzi wa dawa za kulevya la Los Tequileros ambalo limekuwa likishtumiwa kwa kuendesha biashara hiyo haramu duniani.

Kufikia sasa taifa la Mexico limerekodi vifo zaidi ya elfu mia tatu arubaini vinavyohusishwa moja kwa moja na ulanguzi wa dawa za kulevya tangu serikali ilipotangaza vita dhidi ya wahalifu hao mwaka 2006.

Inaaminika kwamba mtandao wa ulanguzi wa dawa za kulevya umekuwa na ushawishi mkubwa kwenye mataifa mbalimbali na hivyo kuwa vigumu kuwakabili watu wanaoendesha biashara hiyo haramu.