Watu watano wameuliwa kwa kukatwa vichwa na washukiwa wa kundi gaidi la Al-Shabaab kwenye Kijiji cha Salama, kata ya Mkunumbi, katika Kaunti ya Lamu.
Miongoni mwa watu waliouliwa ni mwanafunzi wa kidato cha tatu ambaye alikuwa ameenda nyumbani kwa ajili ya likizo ya katikati ya muhula.
Inaarifiwa kwamba uvamizi huo ulifanyika saa saba usiku wa kuamkia leo, ambapo watano hao waliamrishwa kutoka nyumba zao kisha kuuliwa.
Inasemekana wanawake waliekezwa katika eneo tofauti walikozuiliwa lakini wakaachiliwa baadaye.
Aidha nyumba kadhaa zimeripotiwa kuteketezwa wakati wa uvamizi huo, mifugo na kuku pamoja na vyakula vilivyokuwa vimehifadhiwa wenye ghala viliibwa.
Mapema leo Kamanda wa Polisi wa eneo la Lamu Magharibi Harrison Njuguna, alisema msako mkali unaendelea ili na hadi sasa hakuna mshukiwa hata mmoja ameripotiwa kukamatwa.
Uchunguzi wa awali unaonesha kwamba mzozo wa ardhi, ndicho chanzo cha uvamizi huo.
Mauaji hayo yamefanyika wiki moja tu baada ya wanajeshi wanane wa KDF kuuliwa katika eneo la Mpaka wa Kenya na Somalia ambapo mmoja wao alizikwa jana kule Bungoma.