×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: NYS ni daraja la wizi wa kura 2017

News

Niliposema mliona kana kwamba nina ajenda dhidi ya serikali. Nilipoyachapisha mlichukulia mambo niliyosema kama dondoo za hapa na pale. Aliposema Raila Odinga baadhi ya wabakaji wa haki za wakenya walituchafulia anga kwa kusema kuwa Raila Odinga ni mfalme wa umaskini. Sasa basi maji yamemwagika.

Kila kukicha majina mapya yanazidi kuchipuka katika sakata hiyo ya NYS huku Josephine Kabura na wenzake wakizidi kumwaga mtama. Anne Waiguru ameamua kufa kijeshi na tai shingoni na wale wote walioramba asali wakidhali asali hulwa kwa umma. Miaka ya nyuma kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale, kiongozi anayesifu kila kitu na kuamini kuwa hata hewa ikichafuliwa na miungu zake midogo midogo ni marashi sasa yeye pamoja na mwenzake Kipchumba Murkomen skauti mwengine anayeonekana kuamini kuwa yanayosemwa na Uhuru na Ruto ni maandiko yake Mungu wamo hatarini

Wawili hawa wametajwa katika kiapo cha Anne Waiguru kwa kutoa huduma tasa na butu. Adan Duale ana sifa za kipekee. Sifa za udhalimu, sifa za kupigia mbuzi gita na kujipiga kifua kila mara wakenya wanapouliza maswali. Adan Duale alituonya wakenya kwa kutaka tujue ya kwamba pesa wakenya wanaozungumzia si za mama zetu.

Duale alituona sisi wapumbavu lakini sasa tunakubaliana naye kwa kusema ndio pesa hizo sio za mama yetu lakini hizi mnazodaiwa kuramba ni za mama zetu. Ni ushuru wetu, ni haki ya kila mkenya minghairi na hayo Kenya ifahamike ni yetu sote na wala sio ya mama zenu pekee. Kwa sasa tuwaache hawa wawili maana nahofia katika siku za usoni watatuambia kuwa kuna visa vya kuenda mbinguni iliyo chini ya serikali ya himaya ya serikali ya Jubilee.

NYS sasa ni kama chama cha uhalifu ama klabu ya majangili wasiojali haki za msingi za wakenya kuishi. NYS kwa kila mkenya ni jumba la wizi, jumba la kamari linalotumiwa kupanga njama ya kuwaibia wakenya. Kila mkenya anajua wazi kuwa NYS ni mkono wa pili wa serikali ya kuiba kura ya mwaka wa 2017. Jameni mnayaona haya ama bado mwafyata domo?

Majuzi vijana wawili ambao ni mara yao ya kwanza kujiandikisha kupiga kura walipata majina yao yamesha-sajiliwa kama wapiga kura kutoka eneo lao la mathare hadi kaunti ya Kiambu, Juja kama wapiga kura. Huu ni ushahidi tosha kuwa NYS huenda imewasaliji mamilioni ya watoto maskini kwa kiegezo cha kuwapa kazi na hivyo basi kuwapigisha kura kinyume na matakwa yao, kinyume na katiba kwa minajili ya majangili wachache wanaotaka uongozi ki-mabavu. Majangili wanaozidi kubaka wakenya kila kukicha.

Suala hili linafaa kuchukuliwa kwa uzito sana na wakenya, mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na viongozi mbali mbali wa upinzani. Singelipenda kuwahusisha viongozi wa kidini maana ni nadra kuwapata. Wao wenyewe wamesahau kuhubiri neon la Mungu na badala yake kuhubiri MENO. Hawamo tena lao kuu ni kunusa makalio ya viongozi wenye hela na hata kujaribu kuwaambia kuwa Mungu anawatambua na kuwapenda sana na uongozi huo wao wa wizi umetokana na baraka zake Mungu.

Hawa ndio mashekhe na wachungaji wa kizazi kipya. Watapeli wakuu wanaoiba kwa jina la Mungu. Hakika haya yote yanayojiri sio demokrasia bali wizi wa hali ya juu. Wakenya na waanze na mapema kutafuta haki zao. IEBC ni simba wa matopeni, simba katuni wa kuchorwa, kuchanwa na kupakwa mafuta na marashi. IEBC haijali wakenya ila inajali maslahi ya wahuni.

IEBC ni sharti ianze na kuangalia usajili wote wa wafanyakazi wa NYS ili wakenya wajue na mapema ni wangapi tayari wamepigishwa kura kinyume na haki zao. IEBC katika makala ya juma lililopita niliwajulisha na kuwataka mfahamu kuwa uongozi wa ki-imla hautakubalika tena Kenya. Uongozi wa kuua na kumwaga damu, uongozi wa kuiba, uongozi wa ufisadi, uongozi wa NYS, uongozi wa Eurobond, uongozi wa Chicken gate, uongozi wa galana, uongozi wa wizi wa ardhi na mali ya umma hautakubalika.

IEBC zimeni maovu ya NYS kabla mambo hayajafikia mbali na kuenda kombo. Zimeni tume wizi ya kimpango ya NYS, zimeni wizi huu maana wakenya sio waganda kukubali maamuzi ya kihayawani. NYS imezidi. NYS inataka kuwatia wakenya tena mimba ya wana-haramu. Wakenya wamechoka na mimba ya miaka mitano. Mimba ya mamba anaengata bila huruma.

Mimba na mzigo kuu kwa wakenya. Tafuteni suluhu ya mambo haya mnayoyapuuza kabla ya mambo kwenda kombo. IEBC ogopeni Mungu jameni. Mungu ni mkuu na daima Mungu atasimama na wanyonge wanaodhulumiwa kwa nguvu za senti. Hizi senti zina mwisho. Hizi senti haziwezi kuzima sauti ya kila mnyonge. Hizi senti mtaziacha papa hapa duniani. Kumbukeni Mungu hana wakati na Majangili wachache. Kenya itashinda hila na ghilba za wahuni madarakani. Mungu ibariki Kenya.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu

 

 

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles