Kwa majuma kadha tumekuwa tukitoa maelezo kuhusu ubora wa maziwa ya mama kwa mtoto mchanga. Katika makala hayo tulisimulia jinsi maziwa hayo yanavyompa kila aina ya manufaa mtoto mchanga, kuanzia kinga ya mwili kuimarika kwake kiumbo na siha kwa jumla na hata uwezo wa kuona vyema hutokana na maziwa ya mama. Pia tumeelezea manufaa anayopata mama kwa kumnyonyesha mwanawe na tukasema kuamwisha huko humfaidi mama kiafya na manufaa mengine mengi ambayo mama mnyonyeshaji hupata.
Ingawa kuna mengi mengine ambayo hatujayasimulia, wiki hii tunatamatisha makala haya ya maziwa ya mama, ili kutoa nafasi kwa akina mama wajifanyie utafiti zaidi wao wenyewe, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanajielimisha juu ya mambo mengi. Kama walivyosema watangulizi wetu, elimu haiishii darasani bali inapatikana mahali popote, na kwa sababu ya vifaa vya kisasa vya mawasiliano na mitandao, mwanadamu anaweza kupata elimu kwa njia mbali mbali, bora awe na nia ya kutafuta elimu.