Ndugu wawili waliosurunda gerezani kwa miaka 22

Diwani wa zamani Choi Keronche alishangaa alipotembelea mji wa Kisii miaka minne iliyopita baada ya kuwa jela kwa miaka 22 jela kwa kosa ambalo anasema kamwe hakulitekeleza. Diwani Keronche aliona jinsi mji wa Kisii ulivyokuwa na majumba makubwa akilinganisha na wakati alipokuwa huko mara ya mwisho mnamo miaka 1990 kabla yeye na nduguye mdogo Francis Chweya kujipata kizimbani wasijue kuwa wangetoka huko wakiwa hai.

Ndugu hao wawili walijionea idadi kubwa ya magari na pikipiki nyingi ambazo zilikuwa zikipeana huduma ya usafiri na huku kila mtu akitumia simu ya rununu kwenye barabara za mji wa Kisii jambo ambalo halikuwa la kawaida wakilinganisha ilivyokuwa hapo awali. Bwana Keronche ambaye aliweza kuhudumu kama diwani wa eneo la Boikanga Mashariki katika eneo bunge la Mogirango Kusini kwa miezi mitano pekee kabla ya kutiwa mbaroni mnamo mwaka wa 1993 kwa madai kuwa walihusika na mauaji ya mama yao wa kambo ambaye aliteketezwa na wanakijiji kwa madai ya kuhusika na uchawi.

“Nilikuwa na umri wa miaka 38 nilipokamatwa na baada ya miaka miwili mimi na ndugu yangu tukahukumiwa kunyongwa na Jaji wa mahakama ya Kisii wakati huo Tom Mbaluto kuhusiana na kuuliwa kwa mama yetu mdogo, ingawa jambo hili lilitekelezwa na umati wa watu,” akasema Bwana Keronche.

Ndugu hao wawili ambao waliachiliwa mnamo Julai 2014 kutokana na msamaha wa Rais wanashanga jinsi watu wanavyotumia mitandao ya kijamii kwa mawasiliano kama vile WhatsApp, Facebook, Twitter na YouTube na marafiki zao nchini na hata kimataifa. Bwana Keronche alisema kuwa  alipokuwa diwani walikuwa wakisafiri hadi mjini Kisii kupiga simu kwenye jumba la Posta lakini kwa sasa anashangazwa kuwa kila mtu awe tajiri au maskini anatumia simu ya rununu ambayo inatiwa mfukoni.

Kupata kiti “Nilichaguliwa kama diwani wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka wa Disemba 1992  ambapo nilikuwa na wapinzani sita na iwapo ningepata nafasi ya kuwahudumia  watu walionichagua kwa muhula huo wote labda ningechaguliwa kama mbunge baadaye,” akasema Bwana Keronche.

Diwani huyo wa zamani pamoja na ndugu yake walikata rufani kwenye mahakama ya rufani ambapo majaji Samuel Bosire, Phillip Tunoi na Richard Kwach walikataa maombi yao na wakalazimika kukamilisha kifungo chao.

 “Ningependa kuiomba serikali kunisaidia kupata mshahara wangu kama diwani kwa muda wa miaka mitano kwa vile kiti changu akikutangazwa kuwa wazi na hakuna uchaguzi mdogo uliofanyika kwa diwani mwingine kuchaguliwa,” akasema Bwana Keronche. Ndugu hao wawili walidumisha msimamo wao kwamba hawakutenda kosa hilo na kwamba walihudumu jela miaka hiyo yote wakisubiri kunyongwa na wamewasamehea wale wote waliowasingizia na kufanya familia zao kuumia miaka yote.

Diwani huyo wazamani anahusisha kukamatwa na kushtakiwa kwake kama njama ya maadui wake kumwangamiza kisiasa kwa vile nyota yake ilionekana kung’aa huku akisema walipata nafasi nzuri pale mama yao wa kambo alipouliwa na umati kwa madai ya kuhusika na uchawi.

“Hatukuamini tulipoelezwa kuwa tunaachiliwa kutokana na msamaha wa Rais huku mimi nikiachiliwa kutoka Jela la Shimo la Tewa mnamo Disemba 2015 na ndugu yangu Chweya akiachiliwa mnamo Julai 2014,” akasema Bwana Choi.

Diwani huyo wa zamani alisema kuwa alipofungwa jela alimwacha  mkewe na watoto wake wanne ambao kwa sasa ni watu wazima huku jambo la kumhuzunisha ni kwamba Nyanyake, Mamake na Binti yake waliaga dunia bila yeye kupata nafasi ya kuwazika.

Bwana Chweya alisema kuwa wanamshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwasemehea kufuatia pendekezo la kamati ya Ushauri ya Kutoa msamaha inayohudumu kwenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ilisema wawili hao walikuwa na nidhamu ya hali ya juu.

Alisema kuwa waliweza kutumikia vifungo vyao katika jela mbalimbali nchini na waliweza kutenganishwa mnamo mwaka wa 2003 pale kifungo chao kilipobadilishwa kutoka hukumu ya kunyongwa hadi kifungo cha maisha ambapo  walikuwa jela tofauti.

Bwana Chweya alisema kuwa familia yao iliwapokea kwa njia nzuri huku wake na watoto wao wakiwa wa msaada mkuu katika jitihada za kuhakikisha kwamba wanajumuika tena kwenye jamii kama raia wema kwa njia rahisi.

“Nawashukuru  sana mke wangu Grace na mke wa ndugu yangu Esther kwa kuweza kuzishikilia familia zetu kwa zaidi ya miaka 20 ambayo tulikuwa mbali na wao huku ikikumbukwa kwamba hatukuwa na tumaini la kuachilia hivi karibuni, “akasema Bwana Chweya.

Uhusiano mbovu Chweya alisema  kuwa hawakuwa na uhusiano mzuri na mama yao wa kambo kutokana ana tofauti za kinyumbani na kwamba hawakuhusika na mauji yake sababu kubwa iliyowafanya watu wafamilia yao kuwakaribisha kwa furaha kwa maana walijua walikuwa watu wazuri.

Ndugu hao wawili ni maseremala waliojifunza taaluma hiyo wakiwa jela ambapo waliweza kutengeneza vifaa vinavyotumika katika majengo ya bunge na ofisi zingine za serikali hata ingawa wanasema hawakupata malipo yoyote kwani vifaa walivyounda vilikuwa mali ya idara ya magereza. Waliomba serikali kuanzisha mpangilio wa wafungwa kulipwa kutokana na kazi wanazozifanya wakiwa jela ili waweze kukimu mahitaji ya familia zao ili hata wakiwa mbali watoto na wake zao wasihumie kwa makosa ambayo hawakutenda.