Tanga Tanga na Kieleweke kumenyana katika Seneti tena

Bunge la Seneti limeratibiwa kufanya vikao maalumu Jumanne na Jumatano wiki ijayo, ili kushughulikia Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Kisiasa mwaka 2021, baada ya kupitishwa katika Bunge la Kitaifa.

Spika Ken Lusaka amesema Kamati ya Shughuli za Seneti itajadili vifungu vya mswada huo kabla ya kutoa mwelekeo rasmi.

Jukumu kuu la Seneti katika mswada huu ni kurasimisha tu mchakato wa bunge katika kuunda sheria, kwani mswada huo umeasisiwa bungeni hivyo kuwa vigumu kufanyiwa marekebisho yoyote katika Seneti.

Wakati wa vikao vya Jumanne na Jumatano wiki ijayo katika Seneti, makabaliano makali yanatarajiwa sawa tu na jinsi ilivyoshuhudiwa katika Bunge la Kitaifa.

Mijadala ya mswada huo imegeuzwa kuwa mashindano ya kupimana nguvu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Iwapo mswada huu utafaulu, basi kutakuwa na uwezekano wa kubuni chama kimoja cha kuleta vyama vingine pamoja, mfano Azimio la Umoja kuwa muungano wa vyama mbalimbali kama vile ODM, Jubilee na DAP-Kenya.

Hata hivyo, hayatakuwapo makubaliano ya muungano jinsi ilivyoshuhudiwa katika NASA, ambapo chama kikubwa kina uwezo wa kuamua mwelekeo wa kisiasa bila kutegemea vyama vidogo vidogo ndani ya muungano.

Bila shaka mrengo wa Tanga Tanga umekuwa ukipinga mswada huo kutokana na ishara kwamba upande wa Rais Kenyatta na Odinga unalenga kubuni muungano miezi sita kabla ya uchaguzi, kisha kuviwekea vikwazo vyama vingine ambavyo vingependa kuungana wakati wowote kabla ya uchaguzi.

Baadhi ya vyama kama vile UDA, ANC, Ford Kenya na Wiper vinashinikiza uhuru wa kubuni miungano bila vikwazo vya kisheria kwani ilivyo sasa, mswada huo unapendelea mrengo wa Raila.

Kwa mujibu wa sheria, kwa sasa hakuna mwanya wa kuwasilisha kesi ya kupinga mswada huo ambao bado unashughulikiwa, kwani kesi inaweza kuibuliwa tu baada ya rais kuidhinisha mswada huo kuwa sheria.

Spika wa Seneti, Ken Lusaka na mwenzake wa Bunge la Kitaifa Justine Muturi watawasilisha mswada huo kwa rais ambaye atautia saini na kuwa sheria, baada ya mabunge yote mawili kukubaliana kuhusu marekebisho hayo.

Kikatiba, mswada huo unatarajiwa kupitishwa miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka huu.