Msajili wa vyama asema Wetangula angali kinara wa Ford Kenya

Msajili wa vyama vya kisiasa Ann Nderitu amesema bado Moses Wetang'ula ndiye Kinara halisi wa chama cha Ford Kenya.

Akizungumza na wanahabari, Nderitu amesema Wetangula ataendelea kuwa kinara wa chama hicho hadi wanachama watakapotatua mgogoro unaoshuhudiwa miongoni mwao.

Aidha, Nderitu amesema sheria zitazingatiwa katika kila mabadiliko yatayofanyika katika chama hicho. Wakati uo huo, Baraza Kuu la Chama cha Ford Kenya limewasilisha orodha ya mabadiliko ya uongozi wa chama kwa Msajili wa Vyama huku Eseli Simiyu akipokonywa wadhifa wa Katibu Mkuu wa Chama. 

Nafasi ya Eseli imechukuliwa rasmi na Chris Wamalwa. Aidha, Wafula Wamunyinyi ambaye aliteuliwa na baadhi ya wanachama ili kuchukua nafasi ya Wetangula na kuwa kiongozi wa chama, amepokonywa wadhifa wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo huku Cynthia Mutere akiteuliwa kuwa kiongozi wa wanawake.

Mabadiliko hayo yameungwa mkono na wanachama arubaini na watatu miongoni sabini na watano wa baraza la chama hicho. Wamalwa ambaye ni Mbunge wa Kiminini ametangaza mabadiliko hayo.

Kauli hii imejiri huku mrengo unaounga mkono mapinduzi yaliyomfurusha Wetangula kutoka uongozi wa Ford Kenya, ukisema umekamilisha mchakato wa kufanikisha utekelezaji wa mabadiliko hayo ambapo Wetangula alipokonywa wadhifa huo.

Wetangula alirithi uongozi wa Ford Kenya kutoka kwa Musikari Kombo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007, ambapo pia chama hicho kilikumbwa na msukosuko sawa na jinsi inavyoshuhudiwa sasa.