Ningali kiongozi wa Ford-Kenya -asisitiza Wetang'ula

Uvutano wa uongozi umezidi katika chama cha FORD Kenya huku Seneta wa Bungoma Moses Wetangula  akisisitiza ataendelea kuwa Kinara  licha ya baadhi ya wanachama kutangaza kubanduliwa kwake.

Akizungumza na wanahabari saa chache tu baada ya kufurushwa kwake kutangazwa, Wetangula amesema mkutano uliofanywa ili kumbandua uliendeshwa kiunyme na sheria.

Aidha, amesema waliohudhuria mkutano wa kumfurusha akiwamo Gavana wa Bungoma Wylliffe Wanamati wataadhibiwa na Kamati ya Nidhamu chamani.

Wetangula amesema alifahamishwa kuwapo kwa njama ya kumbandua bila kufuata sheria, na hata Naibu Kiongozi wa Ford Kenya Richard Onyongwa kushawishiwa kupewa fedha na mahasimu wake ili kufanikisha mpango huo.

 

Wakati uo huo, Wetangula ametangaza mabadiliko katika uongozi wa Ford Kenya, akimpokonya Eseli Simiyu wadhifa wa Katibu Mkuu wa Chama na kumpa nafasi hiyo Chris Wamalwa ambaye alipokonywa wadhifa wa Kinara wa Wachache Bungeni.

Wamunyinyi ambaye alikuwa ameteuliwa kuchukua nafasi ya Wetangula amefurushwa pamoja na Eseli kutoka kamati ya kitaifa ya chma hicho, na nafasi zao kuchukuliwa na Catherine Wambilianga na Vincent Gimose.