Wanawake wapongeza ushirikiano baina ya Kenyatta na Gideon Moi

Chama cha Maendeleo ya Wanawake humu nchini kimepongeza mabadiliko ambayo yametekelezwa katika uongozi wa Chama cha Jubilee katika Bunge la Seneti.

Viongozi wa chama hicho aidha wamesifia ushirikiano mpya baina ya Chama cha Jubilee na Kanu wakisema kuwa ushiriano huo utaleta mwelekeo katika siasa za humu nchini.

Wakizungumza na wanahabari, viongozi hao wanasema kwamba hatua ya Rais Uhuru Kenyatta na Seneta wa Baringo Gideon Moi kuunda muungano italeta amani nchini.

Aidha wanawake hao wamewakashifu Wabunge wa Kike wanaoegemea mrengo wa Naibu wa Rais William Ruto chini ya Mwavuli wa Inua Mama wanaopinga mabadiliko hayo na kufurushwa kwa maseneta watano maalumu. Viongozi hao wakiwamo Aisha Jumwa na Alice Wahome jana wameendeleza shutma dhidi ya Jubilee wakikashifu kutimuliwa kwa  Maseneta Kipchumba Murkomen na Susana Kihika.

Wametoa wito kwa viongozi wa Inua Mama  na wengine kuheshimu uongozi wa nchin na kukomesha matamshi ya kudhalilisha uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Wakati uo huo wamependekeza kushirikishwa kikamilifu katika juhudi za kupambana na janga la korona.