Maseneta wanahangaisha magavana bila sababu

Maseneta hawapaswi kuwashtumu magavana kufuatia ufujaji au wizi wa fedha za umma kabla hawajatathmini vyema ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, amesema Gavana wa Pokot Magharibi, Profesa John Lonyangapuo.

Akizungumza na Radio Maisha, Lonyangapuo aidha amewasuta maseneta kwa kuhusishwa na ufisadi ilhali hawana ushahidi.

Aidha gavana huyo amesema maseneta hawajakuwa wakitekeleza majukumu yao ya kuhakikisha kaunti zinatengewa fedha za kutosha, badala yake kuwapiga vita magavana.

Wakati uo huo, Lonyangapuo ameelezea utayarifu wake atakapofika mbele ya Kamati ya Seneti ya Uhasibu tarehe 29 mwezi huu kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha za kaunti yake. Amewaonya maseneta dhidi ya kumuuliza maswali ambayo hayahusiani na serikali yake.

Ikumbukwe magavana wote ambao wamehojiwa wamekuwa wakikumbwa na wakati mgumu kuieleza kamati hiyo jinsi fedha zilivyotumika katika kaunti zao.

Related Topics

Lonyangapuo Pokot