DCI wanzisha uchunguzi dhidi ya mameneja na makamishna wa Kra.

Maafisa wa DCI wanaochunguza sakata ya ukwepaji kulipa kodi katika Mamlaka ya Ukusanyaji Kodi, KRA sasa wameanzisha uchunguzi dhidi ya mameneja wakuu na makamishna wa Mamlaka hiyo.

Mkuu wa DCI George Kinoti amesema kwamba uchunguzi huo hautamsaza yeyote na kwamba lengo kuu ni kuwaajibisha maafisa hao ambao wamelemaza lengo la serikali kukusanya mabilioni ya fedha kutoka kwa walipa kodi.

Msako huo unajiri wakati maafisa 41 wa KRA waliotiwa mbaroni Ijumaa wiki iliyopita wakitarajiwa kuwasilishwa mahakamani baadae leo wakikabiliwa na mashataka mbalimbali ya ufisadi. 

Maafisa hao hao ni miongoni mwa 75 wanaolengwa kufikishwa mahakamani wakituhumiwa kutumia mbinu mbalimbali kuwasaidia watu kukwepa kulipa kodi. Aidha, Idara ya Upelelezi, DCI imewataka maafisa wengine zaidi ya thelathini kujisalimisha katika Makao Makuu ya DCI leo kufikia saa moja asubuhi.

Kwa wikendi nzima, maafisa hao wengi wakiwa wa ngazi ya chini wamezuiliwa katika vituo vya polisi vya Parklands, Kilimani na Central wakihojiwa kuhusu madai hayo.