Jonathan Toroitich Moi mwanawe wa kwanza wa Rais Mstaafu Moi, amefariki dunia

Familia ya Rais Mstaafu, Daniel Arap Moi inaendelea kuomboleza kufuatia kifo cha mwana wa rais huyo mstaafu, Jonathan Toroitich. Jonathan atakumbukwa kwa kushiriki mashinadani ya magari ya safari rally pamoja hasa wakati wa sherehe za Pasaka. Tayari viongozi mbalimbali wameanza kutuma risala za rambirambi kwa familia ya Rais huyo mstaafu. Rais Msytaafu Mwai Kibaki anewaongoza viongozi mbalimbali kutuma risala za rambirambi.

 Katika taarifa ya familia iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Seneta wa Baringo, Gideon Moi, familia hiyo imemtaja Jonathan kuwa atakayekumbukwa na wengi kwa kushiriki mbio za mashindano ya safari rali kwa miaka mingi ambayo mara nyingi yaliandaliwa wakati wa sherehe za pasaka. Hii hapa sauti ya magari yaliyoshiriki mashindano hayo.

Jonathan vilevile anajulikana kuwa mkulima japo alizingatia kujihusisha na masuala binafsi baada ya kuacha kushiriki mashindano ya Safari Rali.

Familia imemtaja kuwa mtu aliyependa kutangamana na watu na asiyekuwa na majivuno. Familia imetoa wito wa Wakenya kuipa muda wa kuomboleza huku ikiahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu mipango itakayoendelea baada ya kifo chake. Katibu wa Mawasiliano, Lee Njiru aidha amesema taarifa zaidi itatolewa hapo kesho.

Jonathan Moi ni nduguye Seneta Gideon Moi, Philip Moi ambaye alikuwa afisa wa jeshi,  Raymond Moi ambaye alihudumu mihula miwili katika wadhifa wa ubunge kwenye Eneo Bunge la Rongai, John Mark Moi ambaye ni pacha wa Doris Moi, Jennifer Jemutai Kositany, na June Moi.

Hayo yanajiri huku viongozi mbalimbali wakituma rambirambi zao kufuatia kifo cha Moi. seneta wa Bungoma Moses Wetangula amesema amesikitishwa na kifo huku akimtaja marehemu kuwa aliyekuwa mpole na aliyekuwa na uhusiano mwema na wote aliojumuika nao.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior amesema Marehemu ataendelea kukumbukwa kwa mchango wake katika mashindano ya Safari Rali.

Chama cha ODM kupitia mtandao wake wa Twitter kimesema kinaiombea familia ya Moi wakati huu mgumu.

Related Topics

KIFO SAFARI MOI