Wakenya milioni 11 wamesajiliwa katika mpango wa Huduma Namba

Jumla ya Wakenya milioni 11 wamesajiliwa katika mpango wa Huduma Namba, siku kumi na sita baada ya usajili huo kuzinduliwa.

Rais Uhuru Kenyatta kupitia mtandao wa Twitter wa Ikulu amesema usajili huo utaendelea kama kawaida hata msimu huu wa sherehe za Pasaka.

Wakati uo huo, Rais amewahakikishia wananchi wanaosajiliwa kuwa data za zi salama na kwamba hawapaswi kuhofia lolote.

Kauli ya Rais inajiri saa chache baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiano Nchini, CA Francis Wangusi kutishia kuwanyima huduma za mawasiliano ya simu watakaokosa kujisajili baada ya muda uliotolewa kukamilika, taarifa ambayo aliikana muda mfupi baadaye.

CA imetilia mkazo taarifa ya Msimamizi wa Kitengo cha Kufanikisha Miradi ya Jubilee katika Ikulu, Nzioka Waita kwamba hakuna atakayeshurutishwa wala kunyimwa huduma za serikali kwa kukosa Huduma Namba. 

 

Hata hivyo, uchanganuzi zaidi wa kauli ya Wangusi unaashiria kuwa huenda ulikuwapo mpango ambao kwa sasa umesitishwa kutokana na ghadhabu za Wakenya dhidi ya kauli hiyo. Ikumbukwe kwamba Katibu Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Gordon Kihalangwa vilevile aliashiria kwamba watakaokuwa wakitafuta huduma za uhamiaji pasi na Huduma Namba watakuwa na wakati mgumu.

Related Topics