SRC kupunguza baadhi ya marupurupu kwa wafanyakazi wa umma

Katika hatua inayolenga kupunguza gharama ya kulipia mishahara ya wafanyakazi wa umma,  Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyakazi hao, SRC imeanza kuondoa baadhi ya marupurupu wanayopewa. SRC imesema inalenga kuondoa jumla ya marupurupu katika vitengo mia moja arubaini na kimoja. Katika awamu ya kwanza tume hiyo imesema kwamba itatathmini marupuruu ya nyumba, likizo na hali ngumu ya kufanyia kazi ili kuhakikisha usawa miongoni mwao, japo huenda yakasalia.

Aidha marupurupu katika vitengo vingine huenda yakaondolewa au kujumuishwa ili kukabili visa ambapo baadhi ya wafanyakazi wa umma wamekuwa wakijinufaisha. Inaarifiwa kuwa wafanyakazi wengi marupuruu hayo ni zaidi ya nusu ya mishahara wanayolipwa hivyo kuilazimu serikali kutumia fedha nyingi katika bajeti yake kuyatosheleza. Hatua hiyo huenda ikaibua mvutano mkali baina ya tume hiyo na wafanyakazi wa umma ambao kwa muda sasa wamekuwa wakipinga kupunguzwa kwa mishahara. Jumla ya wafanyakazi laki saba na hamsini wa serikali kuu, zile za kaunti na idara mbalimbali wanatarajiwa kuathirika na mpango huo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa ARC Lyn Mengich, hatua hii inafuatia tathimini ya mishahara ya wafanyakazi wa umma iliyofanywa chini ya mtangulizi wake, Sarah Serem. Utafiti uliofanywa na SRC, unaonesha kwamba serikali hutumia asilimia 70 ya fedha zilizotengewa mishahara ya wafanyakazi wa umma kulipia marupuruu.

Ikumbukwe kila mwaka jumla ya shilingi bilioni saba hutumika kulipia mishahara ya wafanyakazi wa umma.