Magavana wamezindua mpango wa kutoa msaada kufuatia baa la njaa

Magavana wamezindua mpango wa kutoa msaada wa fedha na vyakula mbalimbali ili kuwasaidia waathiriwa wa baa la njaa kwenye kaunti zinazoathiriwa na ukame.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Wycliffe Oparanya amedokeza kwamba kila kaunti nchini itatoa shilingi milioni moja ili kuzisaidia kaunti 17 ambazo zimeathirika zaidi.

Akizungumza wakati wa kuzindua mpango huo, Oparanya ambaye pia ni Gavana wa Kakamega ameishtumu serikali kuu kufuatia madai kwamba hakuna aliyefariki dunia kutokana na makali ya njaa.

Wakati uo huo, Gavana wa Tharaka Nithi, Muthomi Njuki ameitaka serikali kuwasambazia waathiriwa mahindi ambayo yamehifadhiwa katika maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka, NCPB. Gavana Muthomi aidha amependekeza waathiriwa kupewa fedha ili kununulia chakula wenyewe, akisema serikali inatumia pesa nyingi katika usafirishaji wa vyakula hivyo hasa kwenye kaunti za Turkana, Pokot Magharibi na Turkana.

Ikumbukwe ni zaidi ya watu milioni 1.2 ambao wanaathiriwa na ukame, ila ni zaidi ya elfu mia nane sitini ambao wameathiriwa zaidi kwenye kaunti 13.

Magavana hao wameyasema haya baada ya mkutano Jumatatu kujadili hali ya ukame kwenye kaunti 17 nchini.