Raila aikosoa serikali kwa kudai kuwa hakuna aliyefariki kutokana na njaa

Huku serikali ikikana kuwa kuna watu ambao wameaga dunia kutokana na baa la njaa, viongozi mbalimbali wakiongozwa na Kinara wa ODM Raila Odinga wamesisitiza kwamba watu wamefariki kwenye maeneo yanayoathiriwa na ukame.

Akizungumza kwenye hafla ya kuchangisha fedha katika Kaunti ya Wajir, Raila aidha amesema viongozi wanaosema hakuna aliyefariki kufuatia makali ya njaa ni adui wa Wakenya.

Amesema serikali inapaswa kushughulikia maslahi ya Wakenya bila kujali maeneo wanakotoka hasa ikizingatiwa wanalipa kodi.

Wakati uo huo, seneta wa Baringo Gedion Moi ameilaumu serikali kwa kutotumia mahindi yaliyo katika magahla yake kuwasaidia waathiriwa wa njaa.

Kuhusu suala la ufisadi ambalo linazidi kuwa kero nchini, Raila amesema watu wanaoiba mali ya umma wanapaswa kukabiliwa kwa mujibu wa sheria.

Amewakosoa viongozi wanaoibua madai kwamba idara za uchunguzi zinawalenga, akisema uhuru wa idara hizo haupaswi kuingiliwa.