Profesa Magoha kuhojiwa

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Waziri Mteule wa Elimu Profesa George Magoha Alhamisi anatarajiwa kuhojiwa na Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, wiki mbili baada ya Rais kumteua.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jumanne wiki iliyopita aliwaeleza wabunge kuwa alipokea barua rasmi kutoka kwa Rais ya kumteua Magoha ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani KNEC.

Kufuatia uteuzi huo, Katibu katika bunge la kitaifa Michael Sialai alitangaza wazi kwa Wakenya kuwasilisha malalamishi yao au mapendekezo kumhusu Magoha kwa siku saba kulingana na katiba ili kulipa bunge muda wa kujadili iwapo aliyekuwa Naibu Mkuu wa chuo kikuu cha Nairobi ana uwezo wa kushikilia wadhifa wa Waziri wa Elimu.

Muturi aliwaagiza wabunge kupitisha au kutulipilia mbali uteuzi wa Magoha kabla ya tarehe 19 Mwezi huu.

Iwapo Magoha ataidhinishwa na Bunge la Kitaifa atakuwa na jukumu la kuhakikisha mtalaa mpya wa elimu umetekelezwa na pia kuhakikisha walimu zaidi wamepata ajira katika shule za serikali ili kuboresha viwango vya elimu baada ya wanafunzi zaidi kuongezeka katika shule za upili kufuatia agizo la serikali ya kuwasajili wanafunzi wote waliyojiunga na kidato cha kwanza.

Ikumbukwe Magoha anachukua nafasi ya Amina Mohammed aliyehamishwa hadi Wizara ya Michezo baada ya mwenzake Rashid Echesa kuachishwa kazi na Rais.

Related Topics