Polisi kwenye Eneo la Ngombeni Kaunti ya Kwale, mapema leo wamevamia nyumba moja inayoaaminika kuwa kituo cha kutoa mafunzo kwa wafuasi wa Kundi la Kigaidi la Al Shabaab na kunasa silaha za uhalifu. Baadhi ya silaha zilizonaswa ni pamoja na panga, visu , mbolea ya kutengeza silaha,viberiti, sare za kijeshi na vitabu vya dini.
Polisi pia wamenasa bendera ya rangi nyeusi na nyeuepe yenye maandishi yanayofungamana na makundi ya kigaidi ya ISIS, Al-Shabaab na Boko Haram .Aidha katika Operesheni hiyo, polisi wamenasa kifaa hatari kinachotumika kutenganeza vilipuzi.
OCPD wa Kwale, Tom Odero, anasema kwamba sehemu hiyo huenda hutumika kutoa mafunzo ya uhalifu .Odero aidha amefichua kwamba maandishi katika bendera hiyo yamefasiriwa kumaansha kwamba '' Tuko tayari kwa vita''. Hata hivyo ,hakuna yeyote aliyenaswa katika nyumba hiyo wakati wa msako huo.
Taifa la Kenya katika siku za hivi maajuzi limekumbwa na mashambulio ya kigaidi, la hivi punde likiwa shambulio la Dusit D2 la Tarehe 15 Januari, ambapo watu 21 walifariki dunia huku wengine wakijeruhiwa.