Jopo la upatanisho lasema limepiga hatua kubwa katika kuwaunganisha Wakenya baada ya Rais Kenyatta na Raila kushirikiana

Huku siku ya Jumamosi wiki hii ikiwa mwaka mmoja tangu kuanza kwa ushirikiano mpya kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga, maarufu Handshake, Naibu Mwenyekiti wa Jopo la Upatanisho lililobuniwa baada ya mwafaka huo, Adams Oloo, amesema jopo hilo limepiga hatua kubwa katika kuwaunganisha Wakenya.

 Jinsi anavyoarifu Mwanahabari wetu Carren Papai, jopo hilo limezuru takribani kaunti 21 kupokea mapendekezo ya Wakenya na washikadau mbali mbali kuhusu mabadiliko wanayotaka nchini kabla ya kuwasilisha ripoti yake.

Akizungumza mapema leo katika Ukumbi wa KICC hapa Jijini Nairobi, Oloo amelipongeza jopo hilo kwa kuendesha mchakato wa kutuliza joto la kisiasa lililosababishwa na uchaguzi tata wa mwaka wa 2017.

Aidha amesema ushirikiano kati ya viongozi hao umefanikisha kwa kiwango kikubwa vita dhidi ya ufisadi kando na kuimarisha uchumi wa kitaifa kufuatia ongezeko la wawekezaji waliokuja kuwekeza nchini.

Wakati wa kikao cha jopo hilo leo hii,  Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, IEBC Wafula Chebukati na Katibu Mkuu wa Ford Kenya Dakta Eseli Simiyu, walipata fursa ya kuwasilisha mapendekezo yao huku wakipendekeza mabadiliko katika Katiba ili kubadili mfumo wa uchaguzi na kuwapa nyadhifa nyingine za uongozi hasa wanaoshindwa katika  kinyang'anyiro cha urais kwa lengo la kuepusha ghasia ambazo hushuhudiwa baada ya uchaguzi.

Chebukati aidha ameilaumu Kamati ya Fedha ya Bunge kwa kufeli katika wajibu wake na kuingilia masuala yasiyokuwa  na umuhimu wakati , IEBC ilipokuwa ikihojiwa kuhusu matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Eseli aidha amesema serikali ina wajibu wa kuongeza mgao wa fedha kwa serikali za kaunti ili kufanikisha maendeleo mashanani.

Related Topics

Uhuru upatanisho