Ndege zilizoratibiwa kutua katika Uwanja wa JKIA zimeelekezwa kutua jijini Mombasa

Ndege zilizoratibiwa kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA zimeelekezwa kutua jijini Mombasa huku zingine zikielekezwa taifa jirani la Tanzania. Hatua hiyo inafwatia mgomo wa Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege, KAA wanaopinga pendekezo la kujumishwa kwa KAA na Shirika la KQ.

Aidha, wanasema kuwa Kenya Airways imekuwa ikirekodi hasara katika mapato yake na hivyo kujumishwa kwao huenda kukaathiri utendakazi wa KAA ikizingatiwa kwamba KQ itasimamisha shughuli zote za usafiri katika Uwanja wa JKIA. Tayari Katibu Mkuu wa KAA Moss Ndiema ametiwa mbaroni huku usafiri ukiendelea kutatizika katika Uwanja wa Ndege JKIA kufuatia mgomo huo. Maelfu ya wasafiri wangali wamekwama tangu saa tisa usiku wakati mgomo uo ulipoanza.

Hayo yakijiri, Waziri wa Uchukuzi James Macharia amewahutubia wanahabari muda mfupi uliopita katika Uwanja wa JKIA na kusema kuwa wakuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege, KAA watachukuliwa hatua kwa kusambaratisha shughuli za usafiri katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini.Macharia amesema kuwa wanagoma wamekiuka agizo la mahakama na kwamba sababu zao za kugoma hazina msingi.

Macharia aidha amesema wizara yake kwa ushirikiano na usimamizi wa JKIA wamefaulu kuitisha usaidizi kutoka idara nyingine za serikali ili kuhakikisha shughuli ya kuwakagua abiria katika uwanja huo inaendelea ikizingatiwa wafanyakazi wanaogoma ni  wale wa ukaguzi wa abiria.

Kwa sasa maafisa wa polisi wanaendelea kuwakabili wafanyakzi hao waliokusanyika ili kudai haki ambayo ni kuzuia kukabidhiwa usimamizi wa uwanja huo kwa Kampuni ya Ndege ya Kenya Airways hatua ambayo wanahofia itasababisha wengi wao kufutwa kazi. Inaarifiwa wafanyakazi sita wa KQ wamejeruhiwa kwenye makabiliano hayo na polisi.

KQ imetangaza kusitishwa kwa safari za ndege kuanzia saa tano hadi wakati hali ya utulivu itakaporejelewa huku waliotarajia kusafiri kuanzia saa tano wakitakiwa kutoelekea katika uwanja huo hadi watakapofahamishwa.

Related Topics

JKIA Mgomo KAA