''Si mimi wa kwanza kufutwa kazi ya uwaziri'' Echesa

Siku moja tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi Rashid Echesa kutoka katika Wizara ya Michezo, Echesa amejitokeza kwa mara ya kwanza na kusema ameridhishwa na uamuzi huo. Amesema anauheshimu uongozi wa rais Kenyatta ambaye ana mamlaka ya kuwateua na kuwafuta mawaziri.

Akipuuzilia mbali mijadala iliyoibuka baada ya kufurushwa kwake, Echesa amewasihi wafuasi wake kuwa watulivu kwani yeye si waziri wa kwanza kutimuliwa.

Haya yanajiri wakati ambapo tayari Waziri mpya wa Michezo na Utamaduni Amina Mohammed, ameahidi kuleta sura mpya ya uongozi katika sekta ya michezo nchini.

Amina ambaye alihamishwa kutoka Wizara ya Elimu na kupewa wadhifa wa Echesa, amemshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa hatua yake ya kumpa jukumu jipya huku akielezea matumaini yake ya kushirikiana na washikadau wote katika kufanikisha maendeleo.

Amempongeza aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la mitihani KNEC George Magoha, kwa utendakazi wake mwema katika baraza hilo huku akimtakia kila la heri katika Wizara ya Elimu.