Gavana wa Benki Kuu amesema kwamba asilimia 99.3 ya Wakenya wana chini ya Sh.1M zilizowekezwa katika akaunti zao.

Na Carren Papai,

Gavana wa Benki Kuu, Patrick Njoroge, amefichua kwamba asilimia 99.3 ya Wakenya wana chini ya Sh.1M zilizowekezwa katika akaunti zao.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Fedha ya Bunge la Kitaifa, Njoroge amewaeleza wabunge kwamba chini ya asilimia 0.7 ya akaunti za benki humu nchini zina zaidi ya shilingi milioni moja. Aidha amekitetea kifungu cha sheria za benki ambacho huagiza kwamba mtu aliye na fedha zaidi ya shilingi milioni moja katika akaunti yake anastahili kutoa maelezo kuhusu fedha hizo akisema sheria hiyo inaendana na sheria za benki kuhusu uhifadhi wa fedha.

Njoroge aidha amesema Taifa liko katika hatari kubwa ya ulanguzi wa pesa, kutokana na kukua kwa haraka kwa sekta ya benki, akisema Benki Kuu i macho kuhakikisha kwamba ufisadi unaoendelezwa kwa njia hiyo unakabiliwa.

Ikumbukwe katika siku za hivi karibuni, baadhi ya benki zimejipata pabaya kwa kuruhusu shughuli za usambazaji wa kiasi kikubwa cha fedha bila kuuliza zilivyopatikana. Katika sakata ya kwanza ya wizi wa fedha katika Shirika la Kitaifa la Huduma za Vijana, NYS baadhi ya benki zilishtumiwa kwa kuruhusu utumaji wa kiasi kikubwa cha fedha uliofanywa na baadhi ya washukiwa wa sakata hiyo hali iliyochangia wizi wa fedha za umma.

Aidha katika kisa kingine, meneja mmoja wa benki anaendelea kuchunguzwa kufuatia kisa ambapo Benki ya Diamond Trust tawi la Eastleigh ilitumiwa na washukiwa wa shambulio la kigaidi kwenye Eneo la 14 Riverside Drive, jijini Nairobi kutuma kiasi kikubwa cha fedha huku benki hiyo ikikosa kuchukua hatua zozote.