Mgomo wa wauguzi Kakamega wasitishwa

Na Beatrice Maganga,

NAIROBI, KENYA, Hatimae mgomo wa wauguzi kwenye Kaunti ya Kakamega umesitishwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi kwenye kaunti hiyo, Bulunya Renson amesema uamuzi huo umeafikiwa ili kutoa nafasi ya mashauriano baina ya wakuu wao na Wizara ya Afya.

Katibu huyo aidha amekana madai kwamba hatua ya kuutisisha mgomo wenyewe imetokana na tishio la Rais Uhuru Kenyatta kwamba wauguzi wanaogoma watafutwa kazi, vilevile kauli ya Kinara wa Chama cha ODM, Raila Odinga kwamba serikali kwa sasa haina fedha za kutosha kutimiza matakwa ya wauguzi.  

Waziri wa Afya kwenye kaunti hiyo, Rachael Okumu amewapongeza wauguzi hao kwa kusitisha mgomo na kusema hatua hiyo inatoa fursa ya kusuluhisha mgomo huo huku wagonjwa wakiendelea kupata huduma muhimu za afya.

Hayo yanajiri huku Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU ukiwashtumu magavana kwa kutoheshimu mkataba wa maelewano uliotiwa saini mwaka wa 2017.

Kwa mujibu wa COTU, wauguzi hawapaswi kulaumiwa hasa ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya magavana ambao wamewalipa wauguzi wao. Wamewalaumu magavana hao kwa kumhusisha Rais Uhuru Kenyatta katika suala zima la wauguzi.

Related Topics

Wauguzi