Wanafunzi miongoni mwa waliouliwa Baringo

Na Esther Kirong,

NAIROBI, KENYA, Imebainika kwamba watu watano ambao wameuliwa katika kijiji cha Kapindasum Lokesheni ya Arabal katika eneo Bunge la Baringo Kusini, wanawajumuisha wanafunzi watatu na polisi wawili wa akiba, KPR.

Chifu wa Kata ya Arabal, William Koech amesema wezi wa mifugo walikivamia kijiji hicho leo alfajiri ambapo waliiba mamia ya mifugo baada ya kutekeleza mauaji hayo.

Kwa mujibu wa chifu huyo, wanafunzi waliouliwa walikuwa katika likizo fupi.

Kamishna wa Baringo, Henry Wafula amesema tayari maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kuwatafuta washukiwa wa mauaji na wizi wa mifugo.

Inaarifiwa maafisa waliouliwa walikuwa wakilengwa na wezi hao ambao wanaaminika kutoka jamii ya Pokot ambao walikivamia kijiji cha Arabal kuwalenga watu wa jamii ya Tugen.

Wezi hao wametorokea eneo la Chepkalacha kwenye Eneo Bunge la Tiaty Mashariki. Viongozi kadhaa akiwamo Mbunge wa Baringo Kusini, Charles Kamuren wameyashtumu mauaji hayo. Kamuren amewashauri maafisa wa polisi kuhakikisha usalama unadumishwa.

Haya yanajiri wiki moja tu baada ya kushuhudiwa makabiliano makali kwenye eneo la Kainuk mpakani pa Kaunti za Turkana na Pokot Magharibi. Watu sita wakiwamo polisi watatu wa akiba, KPR waliuliwa kwenye mapigano hayo baina ya jamii ya Pokot na Turkana.

Aidha afisa mmoja wa polisi na mvulana wa umri wa miaka 15 walijeruhiwa wakati wa makabiliano hayo.

Related Topics