'Msinipake doa', aonya Waziri Balala

Na Caren Omae,

NAIROBI, KENYA, Waziri wa Utalii Najib Balala amejitetea dhidi ya madai ya ufisadi katika wizara yake.

Akizungumza alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Michezo, Utalii na Utamaduni, Balala amezifutilia mbali taarifa kwamba alihusika katika utoaji tenda ya shilingi milioni moja kwa kampuni ya The American Society of Travel Agents ili kutoa huduma ambazo hazijabainishwa wakati wa maonesho yaliyofanyika katika jumba la KICC, Nairobi, 2016/ 17. 

Waziri huyo amesema shughuli ya utoaji zabuni haikufanyika ilivyodaiwa.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba uchunguzi umekuwa ukiendelea kuhusu madai hayo kwa kipindi cha miezi sita iliyopita na kusema kwamba amekuwa akishirikiana na EACC katika uchunguzi huo.

Ameendelea kukana madai kwamba Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC ilifanya msako nyumbani kwake, wiki jana kuhusu madai hayo.

Wakati uo huo, Balala amesema hakuna shughuli ya utoaji tenda iliyofanyika baina ya Wizara yake na kampuni hiyo kwani umekuwa ushirikiano wa kuandaa warsha mbalimbali nchini.

Amesema alifanya mkutano na EACC jana ambapo aliwaeleza kuhusu madai hayo yanayoibuliwa kuhusu wizara yake.

Awali iliarifiwa kuwa EACC iliingilia kati suala hilo baada ya kubainika kwamba Balala mwenyewe ndiye aliyesaini mkataba kuhusu kandarasi hiyo iliyotolewa moja kwa moja bila kupitia njia ya ushindani, badala ya kusainiwa na afisa wa Kitengo cha Uhasibu katika wizara yake. 

Related Topics

Balala