Ibada ya wafu kwa ajili ya mwanaharakati Mwatha kufanyika Alhamisi

Na Sofia Chinyezi,

NAIROBI, KENYA, Ibada ya wafu kwa ajili ya Mwanaharakati wa kutetea Haki za Binadamu Caroline Mwatha itafanyika katika eneo la Freedom Corner, kwenye Bustani ya Uhuru Nairobi.

Mwili wa Mwatha ulipatikana kwenye Hifadhi ya Maiti ya City atazikwa katika eneo la Asembo katika Kaunti ya Siaya, tarehe ishirini na tatu yaani Jumamosi. Awali Mwatha alidaiwa kuuliwa na maafisa wa polisi ila uchunguzi ukabainisha kwamba aliaga dunia alipojaribu kuavya mimba.

Ikumbukwe baadhi ya maswali yalikuwa yakiibuliwa awali kufuatia mauaji tata ya Caroline lakini yakapata uvumbuzi baada ya upasuaji uliofanywa katika Hifadhi ya Umash.

Baadhi ya maswali hayo yalihusu uhalisia wa taarifa ya polisi kwamba Mwatha alikuwa mja mzito na iwapo ingewezekana kusubiri hadi miezi mitano kabla ya kuamua kuavya mimba. Madai hayo vilevile yalitaja baadhi ya majeraha aliyokuwa nayo ambayo sasa imebainika alikatwa ili kuweka dawa za kuhifadhi mwili.

Kadhalika, madai mengi yalilimbikiziwa idara ya polisi hasa kufuatia kazi aliyokuwa akiifanya Mwatha ya kuwatetea vijana na kupinga mauaji ya kiholela katika mtaa wa Dandora.

Uchunguzi sasa utaendelezwa kwa waliotiwa mbaroni wakiwamo wasimamizi wa Kituo cha Afya cha New Njiru Community Centre  na jamaa aliyetajwa kuwa na uhusiano naye Alexander Gitau. 

Related Topics

Mwatha