Rais Kenyatta awasuta wafanyakazi wa umma wanaogoma kila mara wakitaka mishahara

Rais Uhuru Kenyatta amewasuta vikali wafanyakazi wa umma wanaogoma kila mwaka kutaka nyongeza ya mshahara na marupurupu bila kujali maslahi ya mkenya mlipa kodi. Rais ambaye amewaongoza viongozi kadhaa akiwamo naibu wake William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga badala yake ametaka washikadau katika sekta ya afya kushirikiana zaidi ili kufanikisha ajenda ya afya bora kwa wote.

Akizungumza kwenye Kaunti ya Kisii, Rais aidha amewataka wauguzi wanaogoma kurejea kazini mara moja huku akisisitiza kauli yake kwamba hakuna pesa za kuwalipa.

Kwa upande wake Kinara wa ODM Raila Odinga, amesema inasikitisha kuona kwamba wagonjwa wanateseka hospitalini ilhali wauguzi wanaendelea kugoma. Amewataka magavana kuwashirikisha kwenye mazungumzo ili kupata mwafaka.

Wakati uo huo, Rais Kenyatta amewataka Wakenya kushirikiana na idara ya mahakama kuhakikisha watu fisadi wanakabiliwa ipasavyo. Ameshikilia msimamo wake wa awali kwamba hakuna yeyote atakayesazwa katika vita dhidi ya ufisadi.

Kauli sawa na hiyo imetolewa na Raila Odinga ambaye ameorodhesha ufisadi kuwa miongoni mwa changamoto kuu ambazo zinahitaji ushirikiano miongoni mwa viongozi na wakenya kwa jumla.

Naibu wa Rais kwa upande wake amewashauri viongozi kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kufanikisha miradi ya maendeleo. Amewataka kuiga mfano wa rais na Raila Odinga kushirikiana kwa manufaa ya Wakenya.

Miongoni mwa miradi ambayo rais amezindua ni wadi mpya yenye vitanda 250, hifadhi ya maiti yenye nafasi ya mili mia moja, eneo jipya la kuzishughulikia familia zinazofiwa, kadhalika nafasi 100 za kuegesha magari katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii.

Rais vivile amezindua ujenzi wa kitengo cha kushughulikia saratani kitachojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.25 ambazo ni ufadhili kutoka Hazina ya Mataifa ya Kirabu kwa Maendeleo Afrika. Vilevile ataanzisha ujenzi wa kitengo cha kuwashughulikia akina mama na watoto na jumba la madaktari wa binafsi. 

Ikumbukwe Chuo Kikuu cha Kisii pia kinatarajiwa kuanza kufunza kozi ya udaktari kutumia Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kisii.

Awali Rais alifanya mkutano ambapo miradi mingine kadhaa ya barabara, uwanja wa ndege wa Suneka, uboreshai wa sekta wa kahawa ilijadiliwa.