watahiniwa wote 12,222 waliopata alama mia nne na zaidi walichaguliwa kujiunga na shule za upili

Wanafunzi takriban elfu mia moja na sita waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, walifanikiwa kubadili shule walizochaguliwa kujiunga nazo na kupata nafasi katika shule walizokuwa wakitaka.

Mabadiliko hayo yalijiri baada ya awali Wizara ya Elimu kusisitiza kwamba ni lazima wanafunzi wajiunge na shule walizochaguliwa kujiunga nazo kupitia Mfumo wa NEMIS. Hata hivyo suala hilo lilipingwa vikali na baadhi ya wazazi ambao wanao walichaguliwa kujiunga na shule za jinsia tofauti huku wengine wakichaguliwa kujiunga na shule ambazo wasingeweza kumudu karo miongoni mwa masuala mengine. Hali hiyo iliilazimu Wizara ya Elimu kulegeza msimamo na kuwaruhusu walimu wakuu wa shule za upili kuwasajili wanafunzi waliobadili shule kupitia Mfumo wa NEMIS.

Usajili wa wanafunzi hao ulianza tarehe 5 mwezi na ulistahili kukamilika tarehe 11 japo muda huo ukaongezwa hadi tarehe 18 mwezi huu baada ya kubainika kwamba wanafunzi takriban laki tatu walikuwa bado hawajajiunga na shule hizo.

Akihojiwa na kamati ya Elimu ya Bunge wiki iliyopita Amina alisema kwamba watahiniwa wote 12,222 waliopata alama mia nne na zaidi walichaguliwa kujiunga na shule za upili. Vilevile wengine waliojiunga na shule hizo ni wanafunzi watano wa jinsia zote walioibuka bora kwenye kila kaunti ndogo.

Related Topics