Ochilo Ayako atwaa ushindi wa useneta Migori

Seneta Mteule Kaunti ya Migori, Ochilo Ayako amewahakikisha wakazi wa kaunti hiyo kwamba atashirikiana nao ili kufanikisha miradi ya maendeleo.
Ochilo amewapongeza wakazi hao kwa kumchagua ili kuwawakilisha katika Bunge la Seneti, huku akiwasihi wapinzani wake kuweka kando tofauti zao kisiasa na kumuunga mkono kwa manufaa ya wakazi wa Migori. Ochilo aidha amewapongeza maafisa wa Tume ya uchaguzi, IEBC kwa kuendesha uchaguzi huo mdogo kwa njia huru na haki.
Kwa upande wake, Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, amesema ni wazi kwamba ODM ina ufuasi mkubwa Migori, kufuatia ushindi wa Ochilo, aliyewania kwa tiketi ya chama hicho.
Aidha Junet amewataka wanaoeneza uvumi kwamba chama hicho hakina demokrasia kukoma, akisema kila chama kina sheria za kuendesha shughuli zake.
Eddy Okech kwa upande wake amewapongeza wafuasi wake kwa kujitokeza licha ya changamoto alizokumbana nazo kutoka wapinzani wake wa ODM. Eddy amesikitia hatua ya viongozi wa ODM kutoka Kaunti nyingine nchini, akisema walitumwa kwenye maeneo bunge yote, hali anayosema ilikuwa njama ya kumdhalilisha. Hata hivyo amewahakikishia wakazi wa Migori kwamba ataendelea kupigania haki zao hata nje ya seneti.
Ochilo ameibuka mshindi kwa kupata kura 85,234 yaani asilimia 57.7 ya kura zote zilizopigwa. Aidha amefuatwa na Eddy Oketh kwa kura 60,555, yaani asilimia 40,99 ya kura zote.
Uchaguzi huo ulifanyika jana kwenye maeneo bunge yote manane kufuatia kifo cha Ben Oluoch aliyefariki dunia baada ya kuugua saratani ya koo. Wagombea wengine wa kiti hicho cha useneta ni Dickson Ogola, Peter Osieko, Samwel Otieno na Solomon Hodo.