Akaunti za benki za Gavana Obado zadhibitiwa

Masaibu yanaendelea kumwandama Gavana wa Migori Okoth Obado, baada ya Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC kuanza uchunguzi wa tuhuma za ufisadi dhidi yake. EACC imezifunga akaunti za benki za gavana huyo, kufuatia madai kwamba jumla ya shilingi bilioni 2.5 pesa za umma zimefujwa katika serikali yake.

Aidha akaunti ambazo zimefungwa ni zile za ndugu zake Obado; Jared Peter Odoyo , Oluoch Kwaga, Ernest Omondi Owino na Joram Opala Otieno.

Vilevile  EACC imebaini kuwa Obado alizihifadhi pesa katika akaunti za wanawe nchini Australia, Hong Kong na Uchina. Tume hiyo imesema huenda ikalazimika kutafuta usaidizi wa kisheria ili kurejesha fedha hizo ambazo zinaaminika kuhifadhiwa katika akaunti mia moja katika mataifa ya nje.

Ikumbukwe Obado ambaye alikamatwa jana, anaendelea kuzuiliwa korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu akikabiliwa na tuhuma za mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo Sharon Otieno.

Related Topics

Migori Akaunti